Arab League yazitaka pande zinazopigana Sudan kuheshimu vipengee vya usitishaji vita
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Arab League ametaka kutekelezwa makubaliano ya kusitisha vita huko Sudan na pande hasimu kuheshimu vipengee vya makubaliano hayo baadaya pande hizo kusaini makubaliano ya kusitisha vita.
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imetoa taarifa leo Jumapili ikitangaza kuwa, Ahmad Abu Gheit Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo amekaribisha kutiwa saini makubaliano ya kusitisha vita kati ya wawakilishi wa jeshi la Sudan na wa vikosi vya usaidizi wa haraka (RSF) na kusisitiza udharura wakutekelezwa makubaliano hayo na pande hasimu zinazopigana huko Sudan kuheshimu vipengee vya makubalino hayo nchini humo.
Taarifa ya Arab League imetolewa baada ya pande zinazopigana huko Sudan kukubaliana kusaini makubaliano ya uistishaji vita wa kibinadamu kwa muda wa wiki moja; makubaliano ambayo yanaweza kuongezwa muda pia.
Usitishaji huu tajwa wa mapigano unaenda sambamba na usambazaji wa misaada ya kibinadamu na kulinda vituo vya matibabu, maji na umeme katika maeneo yaliyoathirika huko Sudan. Mapigano ya silaha yalianza Sudan tangu Aprili 15 mwaka huu kati ya vikosi vya jeshi na vikosi vya usaidizi wa haraka kuhusu uongozi wa nchi.
Karibu watu elfu moja wameuliwa na wengine kaibu 5,300 wamejeruhiwa na takribani milioni moja wamekuwa wakimbizi tangu kuanzia vita huko Sudan mwezi Aprili mwaka huu hadi sasa.