Ghasia zashtadi Senegal, mitandao ya kijamii yafungwa
Watu kadhaa wameuawa huku wengine wengi wakijeruhiwa nchini Senegal, katika maandamano ya ghasia ya wafuasi wa kiongozi wa upinzani nchini humo Ousmane Sonko, ambaye karibuni alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.
Mapambano baina ya wafuasi wa upinzani na askari polisi yamesababisha vifo vya watu wasiopungua tisa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Machafuko mapya nchini Senegal yalianza Alkhamisi iliyopita baada ya Sonko mwenye umri wa miaka 48 kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya 'kuwafisidi vijana'. Sonko ambaye amefutiwa shitaka la ubakaji lililokuwa linamkabili, binafsi hakuwa mahakamani wakati wa hukumu hiyo.
Harakati ya Kutetea Demokrasia inayojumuisha pia makundi ya asasi za kiraia, imetoa mwito wa kuendelea kufanyika maandamano hayo ya kulalamikia hukumu hiyo wanayoitaja kuwa ya kisiasa.

Ousmane Sonko, ni mwanasiasa mwenye umaarufu mkubwa kwa tabaka la vijana nchini Senegal, anaonekana kutoa upinzani mkubwa kwa Rais Macky Sall licha ya kushika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2019.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Senegal, Antoine Félix Diome amesema serikali imebana mitandao ya kijamii, ili kuzuia usambazaji wa jumbe za chuki na kichochezi wakati huu wa fujo.
Wananchi wa Senegal hasa vijana wameghabishwa na hatua hiyo ya kufungwa kwa mitandao ya Facebook, Instagram, Messenger, Telegram, TikTok, WhatsApp na YouTube.