MSF yatahadharisha: Ugonjwa wa kipindupindu unaenea kwa kasi kubwa nchini Kenya
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limetangaza kuwa kipindupindu kinaenea kwa kasi miongoni mwa watu waliokimbia makazi yao wanaoishi katika kambi za wakimbizi nchini Kenya.
Timu ya Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka imetangaza kuwa zaidi ya watu 2,700 wameugua kipindupindu katika kambi tatu za Kaskazini Mashariki mwa Kenya.
MSF ilikuwa imetangaza kuwa watu wawili wameaga dunia kutokana na maradhi ya kipindupindu.
Mmoja wa madaktari wa MSF ametangaza kuwa kambi hizi zinawapa hifadhi watu 300,000 waliokimbia makazi yao, wengi wao wakiwa ni kutoka nchi jirani ya Somalia.
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limetangaza kuwa kambi za wakimbizi nchini Kenya zinahitaji maji safi ya kunywa, sabuni na bafu zaidi, na kwamba kwa upande mwingine, tatizo la taka katika kambi hizo lazima litatuliwe.
Mjumbe wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, Abigail Lockhart amesema kutokana na hali mbaya ya kiafya, haiwezekani kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kwa kutumiia chanjo, na kwamba kambi hizo zimesababisha kuenea kwa magonjwa kama surua na kipindupindu.
Hassan Maiyaki, mkuu wa Madaktari Wasio na Mipaka nchini Kenya, hivi karibuni alielezea wasiwasi wake kuhusu hali ya afya katika kambi ya Dadaab na kusema: Hali hii imekuwa mbaya kupita kiasi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kama hatua za haraka hazitachukiliwa kwa ajili ya kutoa maji safi na huduma za afya kwa wakimbizi, tutakabiliwa na janga la kibinadamu.