UN yalaani shambulizi la kigaidi Uganda, waliouawa ni zaidi ya 40
(last modified Sun, 18 Jun 2023 07:45:32 GMT )
Jun 18, 2023 07:45 UTC
  • UN yalaani shambulizi la kigaidi Uganda, waliouawa ni zaidi ya 40

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani vikali shambulizi la kigaidi lililoua makumi ya wanafunzi katika eneo la Mpondwe, magharibi mwa Uganda.

Farhan Haq, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema Guterres amemshtushwa na shambulizi hilo la kinyama dhidi ya shule moja katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Amesema Katibu Mkuu wa UN ameguswa na ukatili huo wa magaidi wa ADF dhidi ya wanafunzi, ambapo amezinyooshea mkono wa pole familia za wahanga wa hujuma hiyo, serikali na taifa hilo kwa ujumla kufuatia unyama huo.

Wakati huohuo, duru za habari zinaarifu kuwa, idadi ya watu waliouawa katika shambulizi hilo la usiku wa kuamkia jana Jumamosi imefika 41, aghalabu yao wakiwa ni wanafunzi.

Msemaji wa polisi ya Uganda, Fred Enanga amesema jeshi la UPDF linawafuatilia wahalifu katika Mbuga ya Taifa ya Virunga. Wanafunzi sita waliotekwa nyara na magaidi hao wenye makao yao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanaripotiwa kuwa katika msitu huo wa Virunga.

Maafisa usalama wakipekua eneo la shambulizi Uganda

Huku hayo yajikiri, Mama wa Taifa, Bi Janet Museveni ambaye pia ni Waziri wa Elimu wa nchi hiyo sanjari na kulaani ukatili huo, amesema familia ya kila mwanafunzi aliyeaga dunia kwenye shambulizi hilo itapewa Shilingi milioni 5 za Uganda kwa ajili ya maandalizi ya mazishi.

Wahalifu walioshambulia shule ya Sekondari ya Lubiriha Ijumaa usiku walipora na kuiba chakula na kuchoma moto mabweni ya shule hiyo iliyoko umbali wa kilomiita 2 kutoka kwenye mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.