Misri yakosoa EU kufuta mkutano baada ya Syria kurejea Arab League
Misri imekosoa uamuzi wa Umoja wa Ulaya (EU) wa kufuta mkutano uliotazamiwa kufanyika wiki ijayo wa ngazi ya mawaziri baina yake na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, kutokana na Syria kurejeshewa uanachama kwenye taasisi hiyo ya Arab League.
Sameh Shoukry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema katika kikao na waandishi wa habari mjini Cairo akiwa pamoja na Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya kwamba, EU inapasa kuheshimu uamuzi uliofanywa na Arab League.
Shoukry amesema, "Uamuzi wa jumuiya unafaa kuheshimiwa na Umoja wa Ulaya, lakini kufuta mkutano wake na Arab League ambao haujafanyika kwa muda wa miaka minne ni jambo la kusikitisha."
Matamshi ya Shoukry yamekuja baada ya Borrell akiwa pamoja na Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuwaambia waandishi wa habari kuwa, mkutano wa ngazi ya mawaziri wa EU na Arab League umeakhirishwa kutokana na Syria kurejea katika jumuiya hiyo ya Waarabu.
Siku chache zilizopita, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, walikubaliana katika kikao cha dharura juu ya suala la Syria kurejeshewa kiti chake ndani ya Arab League.
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilisimamisha uanachama wa Syria, mmoja wa wanachama waanzilishi, mwezi Novemba 2011, kwa madai kuwa eti Damascus ilikuwa inakandamiza maandamano ya upinzani. Syria ililaani hatua hiyo wakati huo na kuitaja kuwa "haramu na ukiukaji hati ya jumuiya."
Sameh Shoukry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema uamuzi wa kuirejeshea Syria uanachama wake umechukuliwa ili kulisaidia taifa la Syria, na kuandaa mazingira ya kurejesha utulivu katika nchi hiyo ya Kiarabu.