Pande hasimu zakubaliana kusitisha mapigano Puntland, Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i99066-pande_hasimu_zakubaliana_kusitisha_mapigano_puntland_somalia
Pande hasimu katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland nchini Somalia zimeafikiana kusitisha mapigano na uhasama.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 22, 2023 02:38 UTC
  • Pande hasimu zakubaliana kusitisha mapigano Puntland, Somalia

Pande hasimu katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland nchini Somalia zimeafikiana kusitisha mapigano na uhasama.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Garowe, vikosi vitiifu kwa serikali na vile vinavyounga mkono upinzani vimekubaliana kusitisha vita, baada ya kushambuliana vikali Jumanne na kusababisha makumi ya watu kuuawa na kujeruhiwa.

Watu wasiopungua 15 waliuawa katika mapigano hayo yaliyosababishwa na suala tata la kuifanyia marekebisho katiba katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland nchini Somalia.

Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia katika taarifa amesema kuwa amesikitishwa na mauaji hayo mjini Garowe, eneo la Puntland. Wazee wa kikabila wanaongoza jitihada za kupatia ufumbuzi mzozo huo kwa njia za amani.

Rais wa Puntland, Said Abdullahi Deni

Wafuasi wa upinzani wanamtuhumu kiongozi wa eneo hilo, Said Abdullahi Deni, kwamba anataka kuifanyia marekebisho katiba kwa shabaha ya kurefuisha kipindi chake cha uongozi kinachopasa kumalizika Januari mwaka ujao.

Mjadala umepamba moto hivi sasa katika Bunge la Puntland kuhusu uwezekano wa kurekebisha katika na kubadilisha mfumo wa uchaguzi katika eneo hilo lililoko kaskazini mashariki mwa Somalia.

Bunge hilo la eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland lilimchagua Said Abdullahi Deni kuwa rais eneo hilo mnamo Januari mwaka 2019, kuchukua nafasi ya Abdiweli Mohamed Ali Gaas.