Jun 30, 2023 03:23 UTC
  • Watu 17 wauawa katika mashambulizi ya kigaidi ya ISIS nchini Mali

Raia wasiopungua 17 wameuawa katika mashambulizi mawili yaliyofanywa na wanachama wenye mfungamano na kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) katika eneo la Gao, kaskazini mwa Mali.

Shirika la habari la Anadolu la Uturuki liliripoti habari hiyo jana Alkhamisi, likimnukuu Hamido Mohamed Bello, Naibu Meya wa mji wa Gabero wenye vijiji vya Gaena na Boya vilivyolengwa kwenye hujuma hizo za wanachama wa kundi lenye mfungamano la ISIS.

Bello amesema raia 14 wameuawa kwa kumiminiwa risasi na magaidi hao katika kijiji cha Boya katika shambulizi la kwanza. Ameeleza kuwa, mbali na watu watatu kuuawa katika hujuma ya pili katika kijiji cha Gaena, wengine kadhaa wamejeruhiwa huku sita wakitekwa nyara.

Afisa huyo wa serikali katika mji wa Gabero kaskazini mwa Mali ameongeza kuwa, wakazi wa vijiji hivyo wameanza kukimbia vijiji hivyo baada ya mashambulizi hayo, na kutorokea katika miji na vijiji salama.

Bello amebainisha kuwa, chanzo cha mashambulizi hayo ni mzozo uliobuka Jumanne baina ya kundi la Daesh katika eneo la Sahara (ISGS), na genge la Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) lenye mfungamano la mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.

Hujua zimeshtadi Mali licha ya uwepo wa MINUSMA

Hii ni katika hali ambayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo Ijumaa linatazamiwa kupiga kura juu ya uwepo wa kikosi cha kulinda amani cha umoja huo nchini Mali, MINUSMA.

Juni 16, Abdoulaye Diop, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali aliishangaza dunia pale alipoutaka Umoja wa Mataifa kuwaondoa haraka iwezekanavyo wanajeshi wake wa kulinda amani wa kikosi cha MINUSMA walioko nchini humo.

Kikosi hicho kilichoasisiwa mwaka 2013, kimekosolewa kwa kushindwa kuwalinda raia dhidi ya mashambulizi ya makundi yenye silaha, licha ya ukubwa wa kikosi hicho na kuwa na bajeti ya kila mwaka ya dola bilioni 1.26.

Tags