Watu 50 wapoteza maisha katika ajali ya barabarani nchini Kenya
Watu wasiopungua 50 wameaga dunia katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea usiku wa kuamkia leo Jumamosi katika kaunti ya Kericho, magharibi mwa eneo la Bonde la Ufa nchini Kenya.
Ajali hiyo iliyotokea Ijumaa mwendo wa saa moja magharibi katika makutano ya barabara ya Londiani, katika barabara kuu ya Nakuru kuelekea Kericho, imehusisha lori lililopoteza mwelekeo, na kugonga matatu tatu za abiria, magari mengine kadhaa ya kibinafsi na pikipiki za boda boda.
Aidha wachuuzi kadhaa waliokuwa pembeni ya barabara hiyo wakiuza bidhaa zao wamepoteza maisha na kujeruhiwa kwenye ajali hiyo. Habari zaidi zinasema kuwa, makumi ya majeruhi wanatibiwa katika hospitali za kaunti za Nakuru na Kericho.
Kamishna wa eneo la Rift Valley, Abdi Hassan amesema watu 48 wameaga dunia kwenye ajali hiyo, na kwamba yumkini idadi hiyo ikaongezeka kutokana na kukwama baadhi ya abiria kwenye mabaki ya magari yaliyohusika kwenye ajali hiyo.
Ajali za barabarani limekuwa janga la muda mrefu nchini Kenya, ambapo kwa wastani nchi hiyo husajili vifo 3,000 vya ajali kwa mwaka.
Februari mwaka huu, watu wasiopungua 14 walipoteza maisha katika ajali nyingine mbaya ya barabarani iliyotokea katika barabara ya Lodwar- Kakuma eneo la Kakwamunyen, kaunti ya Turkana, kaskazini magharibi mwa Kenya.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO, ajali za barabarani ndizo zinazoongoza kwa vifo vya vijana wa bara la Afrika; hivyo serikali katika bara zimetakiwa kuchukua mwelekeo mpya wa pamoja wa kukabiliana na tatizo hilo.