Jul 01, 2023 09:53 UTC
  • Burkina Faso yasimamisha matangazo ya kanali ya LCI ya Ufaransa

Serikali ya Burkina Faso imesimamisha kwa muda matangazo ya kanali ya habari ya Kifaransa ya LCI kwa madai ya kutangaza habari za uwongo na upotoshaji.

Baraza Kuu la Mawasiliano nchini humo (CSC) limekosoa matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na mwanahabari wa kanali hiyo, Abnousse Shalmani, kuhusu harakati za magenge ya kigaidi.

Baraza hilo limesema, mwanahabari Shalmani alitangaza habari ya upotoshaji mnamo Aprili 25 mwaka huu, akidai kuwa magaidi wanasogea mbele kwa kasi, na eti wanajeshi wa serikali wanawatumia raia kama ngao kujikinga na hujuma za magaidi.

Baraza Kuu la Mawasiliano nchini Burkina Faso limesimamisha kwa miezi mitatu matangazo ya kanali ya habari ya Kifaransa ya LCI nchini humo kwa kutangaza na kueneza habari hizo za uwongo na upotoshaji.

CSC imesema mwanahabari huyo wa shirika la Kifaransa la LCI pasi na kutoa ushahidi na kuanisha chanzo cha ripoti yake, alidai kuwa asilimia 40 ya ardhi ya Burkinabe inashikiliwa na magaidi, na eti serikali inatumia raia 90,000 wa kujitolea kulinda wanajeshi wa nchi hiyo dhidi ya mashambulizi ya magaidi.

Stesheni za Ufaransa zimekuwa zikifungiwa Afrika Magharibi kwa kutangaza propaganda

Mwishoni mwa mwaka jana, serikali ya Burkina Faso ilisimamisha nchini humo matangazo ya Redio ya Kifaransa ya RFI inayofadhiliwa na serikali ya Paris, kwa madai ya kutangaza habari za uwongo na kuyapa jukwaa na sauti magenge ya kigaidi.

Aidha Machi mwaka jana pia, nchi nyingine ya Afrika Magharibi, Mali, ilichukua hatua ya kusitisha nchini humo matangazo ya Redio ya Kifaransa ya RFI na televisheni ya France 24 kwa tuhuma kuwa vyombo hivyo vya habari vinaripoti habari za uwongo na upotoshaji. 

Tags