Kushadidi mivutano ya kisiasa baina ya Ufaransa na utawala wa Kizayuni
Utawala wa Israel umefuta viza za wabunge na maafisa 27 wa Ufaransa wa mrengo wa kushoto siku mbili kabla ya safari yao ya kuelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu iliyopewa jina bandia la Israel.
Hatua hiyo pia imekuja siku chache baada ya Tel Aviv kuwapiga marufuku wabunge wawili wa Uingereza kutoka chama tawala cha Labour kuingia Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Israel ilitangaza kufutwa kwa viza za watu hao chini ya sheria inayoruhusu mamlaka kupiga marufuku kuingia kwa watu ambao wanaweza kuchukua hatua dhidi ya Israel. Wanachama 17 wa kundi lililopanga kusafiri katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, wanatoka katika vyama vinavyounga mkono mazingira na ukomunisti. Kundi hilo limesema kuwa ni wahanga wa "adhabu ya pamoja" ya Israel na kumtaka Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuingilia kati.
Walisema katika taarifa kwamba, wamepokea mwaliko kutoka kwa ubalozi mdogo wa Ufaransa huko Baytul-Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu kufanya ziara ya siku tano. Waliongeza kuwa wanapanga kutembelea maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na maeneo ya Palestina kama sehemu ya dhamira yao ya "kukuza ushirikiano wa kimataifa na utamaduni wa amani."
Hatua hiyo ya Tel Aviv inakuja huku kukiwa na mvutano wa kidiplomasia na baada ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kusema kuwa hivi karibuni Paris itatambua taifa huru la Palestina. Macron alielezea matumaini yake kuwa, uamuzi wa Ufaransa kulitambua taifa la Palestina utazihamasisha nchi nyingine kuchukua hatua kama hiyo.

Rais wa Ufaransa alitangaza katikati ya mwezi huu wa Aprili kwamba, nchi yake inaweza kuitambua nchi huru ya Palestina Juni ijayo sabamba na kufanyika mkutano kuhusu Palestina huko New York, kitendo ambacho kilimkasirisha Netanyahu. Hadi sasa nchi ya Palestina imetambuliwa na takriban nchi 150 duniani, ingawa nchi nyingi kubwa za Magharibi, zikiwemo Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Japan bado hazijachukua hatua hiyo.
Matamshi ya Macron yalikabiliwa na majibu hasi kutoka kwa Netanyahu, ambaye alijibu kwa hasira uwezekano wa Ufaransa kulitambua taifa la Palestina, akisema kwamba kuanzishwa kwa taifa la Palestina kando ya Israel kutakuwa "tuzo kubwa kwa ugaidi."
Nchi za Ulaya zimekuwa zikiegemea upande wa utawala wa Kizayuni tangu mwanzoni mwa vita vya Gaza, na wakuu wa nchi kama Ujerumani, Ufaransa na Uingereza wamesafiri hadi Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuunga mkono hadharani vita vya kikatili vya Israel na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina. Umoja wa Ulaya pia ulichukua mkondo wa kuunga mkono utawala wa Kizayuni katika miezi ya kwanza ya vita.
Hata hivyo, baada ya mwaka mmoja wa vita vya Gaza na baada ya kufichuliwa mauaji ya halaiki ya watu waliodhulumiwa wa Gaza, hasa wanawake na watoto, pamoja ubomoaji na uharibifu mkubwa dhidi ya Gaza, na kuzuia kwa Israel kupelekwa misaada kwa watu wa Gaza kwa lengo la kusababisha njaa na kifo cha taratibu cha wakazi wote wa eneo hili lililokumbwa na vita, Umoja wa Ulaya ulilazimika kuchukua msimamo wa ukosoaji kuhusiana na hili. Suala hili lilibainishwa na Josep Borrell aliyekuwa Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya wakati huo.
Serikali ya Ufaransa kwa kutilia maanani mashinikizo ya ndani ya nchi kama vile maandamano makubwa na kuongezeka upinzani wa vyama vya mrengo wa kushoto vya nchi hiyo kutokana na kuendelea vita vya Gaza na vilevile ili kudumisha uhusiano na nchi za Kiarabu, ililazimika kuukosoa utawala wa Kizayuni wa Israel na kutoa wito wa kusitishwa vita katika Ukanda wa Gaza.
Katika mazungumzo yake ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Aprili 15, Macron alisisitiza haja ya kusitishwa mara moja vita katika Ukanda wa Gaza pamoja na kupokonywa silaha Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Macron pia alitoa wito wa kutoa fursa muhimu kwa utatuzi wa kisiasa kwa msingi wa suluhisho la nchi mbili. Ufaransa imeunga mkono mpango wa nchi za Kiarabu, ikiwemo Jordan, wa kujenga upya Gaza bila kuwafukuza wakazi wake milioni 2.4.

Mpango huo ambao pia unaungwa mkono na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, unapinga pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump la kuwahamisha wakazi wa Gaza hadi Jordan na Misri. Macron pia alisisitiza kuwa ni muhimu kabisa kufungua vivuko vyote kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kwa raia wa Gaza, na kutoa wito wa kukomeshwa kwa "mateso" ya raia katika eneo hilo lililozingirwa.
Licha ya ukemeaji na matamshi ya kulaani ya kidhahiri dhidi ya Israel na vilevile kutolewa matakwa ya kuhitimisha vita na kutumwa misaada ya kibinadamu katika eneo lililoharibiwa na vita la Gaza, lakini Umoja wa Ulaya na mataifa yanachama ikiwemo Ufaransa, yamekuwa yakijizuia na hatua yoyote ile ya kuifanya Israel iache kutenda jinai zake huko Gaza.
Kwa muktadha huo, inawezekana kusema kuwa, madola ya Ulaya tofauti na Marekani ambayo daima huiunga mkono Israel katika hali yoyote ile pamoja na jinai zake, yakiwa na lengo la kulinda hadhi na heshima yao yamekuwa yakiukosoa utawala ghasibu wa Israel katika fremu ya kutoa nara za haki za binadamu. Lakini pamoja na hayo kimsingi hiyo ni danganya toto kwani madola hayo hayachukui hatua yoyote athirifu kama kuiwekea Israel vikwazo vyenye taathira. Si hayo tu, bali baadhi ya madola ya Ulaya kama Ujerumani yamekuwa yakiipatia silaha Israel kwa kisingizio cha kukabiliana na Hamas.