Wakodivari wanataka mabadiliko ya Katiba
Jumuiya za kiraia nchini Ivory Coast zimeafiki suala la kufanyika marekebisho ya katiba ya nchi hiyo kwa ajili ya kutayarisha mazingira ya kufanyika uchaguzi sahihi nchini kote.
Marie Paule Kodjo ambaye ni mwanachama wa Jumuiya ya Kiraia ya Ivory Coast na msimamizi wa uchaguzi nchini humo amesema kuwa, jumuiya za kiraia zinataka kuimarishwa demokrasia kwa kufanyiwa marekebisho katiba na kuitisha uchaguzi huru na wa haki.
Katika miezi ya Septemba na Oktoba mwaka huu wananchi wa Ivory Coast wanatazamiwa kushiriki katika kura ya maoni ya marekebisho ya katiba ya nchi hiyo. Baada ya kura hiyo ya maoni kutafanyika uchaguzi wa serikali za mitaa na baadaye uchaguzi wa Bunge.
Nchi ya Ivory Coast ilitumbukia katika machafuko makubwa ya ndani na mgogoro wa kisiasa hususan katika miaka ya 2010 na 2011. Oktoba mwaka 2015 Rais Alassane Ouattara alianza kipindi cha pili cha uongozi wake katika jitihada za kuimarisha usalama na amani nchini humo.