Wahajiri kadhaa watoweka baada ya boti yao kuzama pwani ya Tunisia
(last modified Sun, 09 Jul 2023 10:58:58 GMT )
Jul 09, 2023 10:58 UTC
  • Wahajiri kadhaa watoweka baada ya boti yao kuzama pwani ya Tunisia

Wahajiri kumi wameripotiwa kutoweka baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka na kuzama katika maji wa Bahari ya Mediterrania, pwani ya Tunisia.

Faouzi Masmoudi, afisa wa mahakama katika mji wa bandari wa Sfax amesema boti hiyo imezama katika pwani ya Zarzis, ikiwa njiani kuelekea Italia. Amesema mtu mmoja amethibtishwa kuaga dunia kwenye ajali hiyo, huku wengine 10 wakiwetoweka.

Afisa huyo wa Idara ya Mahakama ya Tunisia ameliambia shirika la habari la Reuters leo Jumapili kuwa, wahajiri wengine 11 wameokolewa na wapigambizi wa Gadi ya Pwani ya Tunisia kwenye tukio hilo.

Televisheni ya al-Jazeera ya Qatar imeripoti kuwa hali ya mamia ya wahajiri wa Kiafrika waliokwama katika eneo la mpaka wa Tunisia na Libya inazidi kuwa mbaya baada ya kufukuzwa na mamlaka ya Tunis kutoka kwenye mji huo wa Sfax, ambao ni wa pili kwa ukubwa katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.

Ripoti ya televisheni ya al-Jazeera imesema mamlaka ya Libya imekataa kuwapoka wahajiri hao waliotimuliwa katika mji wa Sfax nchini Tunisia na kutelekezwa jangwani.

Safari hatarishi za wahajiri kwenda Ulaya

Tunisia iko kwenye eneo la katikati mwa Bahari ya Mediterania, na ni moja ya njia kuu zinazotumiwa na wahamiaji haramu wenye tamaa ya kufika barani Ulaya. 

Wimbi la uhamiaji haramu kutoka pwani ya Tunisia kuelekea nchini Italia kwa kawaida huongezeka wakati wa kiangazi kwa sababu ya hali nzuri ya hewa.