Wahajiri 300 kutoka Senegal wahofiwa kufa maji wakielekea Uhispania
(last modified Tue, 11 Jul 2023 07:14:08 GMT )
Jul 11, 2023 07:14 UTC
  • Wahajiri 300 kutoka Senegal wahofiwa kufa maji wakielekea Uhispania

Mamia ya wahajiri wanahofiwa kupoteza maisha baada ya boti tatu walizokuwa wakisafiria kuelekea Uhispania kutoweka baharini.

Helena Maleno Garzon, Mratibu wa shirika la misaada ya kibinadamu la Walking Borders amesema boti hizo hazijakuwa na mawasiliano na yoyote tangu ziondoke katika mji wa pwani wa Mbour, katikati ya Senegal mnamo Juni 23. 

Garzon ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, boti mbili zilizokuwa zimebeba watu 100 ziliondoka Mbour, yapata kilomita 100 kutoka Dakar mji mkuu wa Senegal Juni 23, huku ya tatu iliyokuwa na wahamiaji karibu 200 ikitokea mji wa kusini wa Kafountine siku nne baadaye.

Ametoa mwito wa kupelekwa ndege kwa ajili ya kutafuta toka angani sehemu ya Bahari ya Atlantic zilikozama boti hizo, ili kusaidia juhudi za kuokoa manusura na kuopoa maiti za wahajiri hao iwapo watakuwa wamekufa maji. 

Wahajiri wakiwa safarini kwenda Ulaya

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la Walking Borders linalofahamika kwa lugha ya Kihispania kama 'Caminando Fronteras', wahajiri zaidi ya wahajiri 800 wamekufa maji au kutoweka wakiwa katika safari hizo hatarishi za kwenda Ulaya katika bahari ya Atlantic katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu.

Wahamiaji wenye ndoto za kuingia Ulaya ambao wengi wao ni kutoka Afrika Magharibi wameongezeka tangu mwanzoni mwa mwaka huu, ikilinganishwa na mwaka 2020 hadi 2022 wakati wa janga la Corona.

Hata hivyo sehemu kubwa ya wahamiaji hao haramu huwa hawafiki wanakokwenda, bali huishia kwenye mikono ya magenge ya magendo ya binadamu na kupigwa mnada masokoni kama watumwa na sehemu nyingine kubwa huzama baharini.