Jul 11, 2023 11:30 UTC
  • Indhari ya Katibu Mkuu wa UN ya kufikia Sudan kwenye ukingo wa vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe

Mapigano nchini Sudan yanaendelea kupamba moto, na juhudi zilizofanywa hadi sasa za kuleta suluhu na kurejesha amani na utulivu katika nchi hiyo sio tu hazijafanikiwa, lakini pande mbili zinazopigana zimeshadidisha pia mashambulizi yao. Kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametahadharisha kuwa, Sudan sasa imeshafika kwenye ukingo wa vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa indhari ya kwamba, vita kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) huenda vikavuruga eneo zima; hali ambayo ni tishio si kwa Sudan pekee bali kwa eneo lote. Aidha Guterres amesema: "Kuna upuuzaji kamili wa sheria za masuala ya kibinadamu na haki za binadamu katika mzozo huu, ambao ni hatari na unasononesha."

Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres

Tangu Aprili 15 hadi sasa, mapigano makali na yaliyotapakaa kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka yamekuwa yakiendelea katika maeneo tofauti ya Sudan, na pande zote mbili zinajaribu kudhibiti vituo muhimu vya nchi, ikiwemo ikulu ya rais, makao makuu ya vikosi vya ulinzi, kamandi ya RSF na baadhi ya viwanja vya ndege vya kijeshi na vya kiraia. Katika mapigano hayo, pandi mbili hasimu zinatumia silaha nyepesi na nzito. Katika baadhi ya maeneo ya mji mkuu Khartoum, zinasikika sauti za miripuko huku ndege za kivita zikionekana kupaa kwenye anga ya jiji hilo. Katika shambulio la karibuni lililofanywa na jeshi la Sudan katika eneo la Dar es Salaam lililoko magharibi mwa Soko la Libya mjini Omdurman, watu 22 wameuawa na mamia ya wengine wamejeruhiwa.

Farhan Haq, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, Guterres ameeleza wasiwasi alionao kuhusu kuenea kwa vita katika majimbo ya Kordofan Kaskazini, Kordofan Kusini na Blue Nile na kubainisha kwamba: sheria za masuala ya kibinadamu zinapuuzwa kwa kiwango hatarishi na cha kutia wasiwasi.

Vinara wa pande hasimu nchini Sudan: Abdel Fattah al Burhan (kulia) na Mohammed Dagalo

 

Pamoja na juhudi zote ambazo zimefanywa hadi sasa kwa madhumuni ya kufanikisha usitishaji vita nchini Sudan, pande zinazopigana hazijaheshimu makubaliano ziliyofikia na mapigano yameendelea kushuhudiwa kati ya pande mbili.

Kwa miaka kadhaa, Sudan imekuwa ikikabiliwa na migogoro mbalimbali ya kisiasa na kiuchumi; migogoro ambayo hatimaye ilipelekea kufanyika mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Omar al-Bashir, dikteta wa zamani wa nchi hiyo. Hata hivyo kuingia madarakani majenerali wa jeshi na kusalia kwenye utawala kwa muda mrefu kulizidisha manung'uniko ya wananchi. Hayo yamejiri sambamba na kushadidi uingiliaji kati wa kigeni, husuan wa madola kinzani, kiasi kwamba katika vita vya sasa, kila moja kati ya pande mbili zinazopigana unanufaika na misaada na uungaji mkono wa madola ya kigeni kwa ajili ya kujidhaminia silaha na zana za kivita.

Kwa upande mwingine, muundo wa kikabila ulioko nchini Sudan, vita na machafuko katika majimbo kama Kordofan na Nile ambayo yamekuwa yakiendelea kwa miongo kadhaa kutokana na maeneo hayo kutengwa na kupuuzwa na serikali kuu, yamepelekea hali ya mambo hivi sasa kuwa mbaya zaidi.

Jarida la Economist limeandika katika ripoti yake: "makabila mengi ya Waarabu wa Darfur, pamoja na ya wenzao weusi yangali yanahisi yanakandamizwa. Vitendo vya ukatili vya Waarabu dhidi ya Waafrika waliorejea huko vimeshamiri".

Justin Musik mfanyakazi wa shirika la misaada la kibinadamu lenye makao yake nchini Ufaransa ambaye alikuwa mjini Al-Janiya anasema: "hivi ni vita vibaya zaidi nilivyowahi kushuhudia katika miaka 20 iliyopita kama mfanyakazi wa misaada. Vidio zilizoko kwenye mitandao ya kijamii zinawaonyesha wapiganaji waliokamia kulipa eneo hilo sura ya Uarabu wakiwashambulia watu na kuwaandama kwa matusi ya kikabila". Kabla ya hapo Folker Peretz, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, alivielezea vita vya Darfur Magharibi kuwa ni "uangamizaji wa kikabila wa kiwango kikubwa".

Masuala ya kiuchumi na nafasi ya kijiografia ya Sudan ni nukta nyingine ambayo imeigeuza nchi hiyo mawindo ya makabiliano ya wazi kati ya makundi ya kisiasa ya ndani na vita vya niaba vya nchi za Kiarabu. Sudan ni nchi muhimu kutokana na kuwepo kando ya Bahari Nyekundu na kuwa na nafasi muhimu kijiografia kwa ajili ya kulifikia eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara na vilevile njia za biashara za kimataifa na mnyororo wa usambazaji kupitia lango la Bab al-Mandab. Kwa upande mwingine, migodi ya dhahabu ya Sudan ni hazina kubwa ambayo nchi zote za eneo pamoja na mawakala wa ndani, wana ndoto ya kuitia mkononi. Mtaalamu wa masuala ya kisiasa Patrick Smith ameandika: "tangu yalipojiri mapinduzi yaliyomng'oa madarakani al-Bashir mwezi Aprili 2019, biashara ya dhahabu ya Sudan imekuwa suala muhimu sana katika siasa za kuwania madaraka ndani ya nchi hii".

Kulingana na nyaraka lilizopata shirika lisilo la kiserikali la Global Witness, Sudan inasafirisha kila mwaka dhahabu yenye thamani ya dola bilioni 16 kuelekea Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) pekee.

Mazingira kiujumla yalivyo hivi sasa yimeiweka Sudan katika hali mbaya sana. Hakuna upande wowote unaowania madaraka nchini humo ulio tayari kufumbia macho maslahi yake binafsi na ya waungaji mkono wake wa nje, na ndio maana juhudi zote zilizofanywa hata za kutekeleza usitishaji vita hazijazaa matunda. Hata hivyo, kila mtu ana wasiwasi, huku ikihofiwa kwamba kuendelea kwa vita hivyo si tu kutaisukuma Sudan na kuifikisha kwenye vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe, lakini nchi zingine za eneo pia zinaweza kujikuta zimetumbukia kwenye lindi la vita hivyo…/

 

Tags