Ulimwengu wa Michezo, Mei 20
(last modified Mon, 20 May 2024 09:31:03 GMT )
May 20, 2024 09:31 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Mei 20

Karibu tukudondolee baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika kona mbalimbali za dunia.

Iran yashinda Taekwondo Asia

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Ubingwa wa Taekwondo ya Asia ya mwaka huu 2024. Wanataekwondo wa Iran wameibuka kidedea baada ya kuzoa medali 3 za dhahabu, 3 za fedha na 3 za shaba kwenye mashindano hayo ya kieneo yaliyofanyika mjini Da Nang nchini Vietnam. Korea Kusini imeibuka ya pili kwa kuchota medali 3 za dhahabu, 2 za fedha na 5 za shaba, huku orodha ya tatu bora ikifungwa na China iliyozoa medali 2 za dhahabu, na fedha 5.

Aidha timu za walemavu za wanataekwondo wa kike na kiume wa Iran zimeibuka washindi kwenye mashindano hayo ya kibara, baada ya kuzoa jumla ya medali 9, zikiwemo 4 za dhahabu, 2 za fedha na 3 za shaba. Waziri wa Vijana na Michezo wa Iran, Kioumars Hashemi, amezipongeza timu hizo za taekwondo za Iran kwa kuipaisha Jamhuri ya Kiislamu kwenye mashindano hayo nchini Vietnam.

 

Katika hatua nyingine, Rais wa Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (FFIRI) Ijumaa hii alitoka nje ya mkutano wa kila mwaka wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA, katika hatua ya kuonyesha kuiunga mkono Wapalestina wanaouawa kwa umati katika vita vya miezi kadhaa vya Israel dhidi ya Gaza. Mehdi Taj na ujumbe wake waliondoka kwenye mkutano wa kila mwaka wa FIFA katika mji mkuu wa Thailand wa Bangkok, huku wakitoa wito wa kusimamishwa Israel kama mwanachama wa FIFA. Taj amesema, "Punde baada ya mwakilishi wa Utawala wa Kizayuni kuingia, mimi na wenzangu tukatoka nje ya ukumbi.

AFC yataka Israel ifukuzwe FIFA kwa jinai zake Gaza

 

Mwakilishi wa Iraq na wawakilishi wa Lebanon, Msumbiji na Algeria pia waliondoka baada yetu." Rais wa FIFA Gianni Infantino amesema chombo hicho kitatafuta ushauri wa kisheria kabla ya kufanya uamuzi kuhusu pendekezo la Palestina la kuifutia Israel uanachama wakati wa Kongamano la Baraza la FIFA mwishoni mwa Julai.

Ligi ya Mabingwa Afrika

Mchezo wa kwanza wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ulishuhudia sare tasa wakati klabu ya Al Ahly ya Misri ilipokabana koo na Esperance de Tunis ya Tunisia wikendi. Esperance de Tunis ikiwa nyumbani, ilishindwa kuonyesha makali yaliyotarajiwa, ikishindwa kupata kona hata moja, huku wapinzani wao, wakipiga kona tatu katika mchezo huo. Esperance ilizuia mashuti mawili katika mchezo huo, ambao ilimiliki mpira kwa asilimia 53, wakati Ahly ikimiliki mpira kwa asilimia 47.

Mechi ya marudiano itafanyika wiki ijayo huko Misri, huku matokeo hayo ya mechi ya kwanza yakiipa faida ES Tunis, kwani sare yoyote ya mabao katika mechi hiyo ya ugenini itawafanya kunyakua ubingwa. Unabashiri nani zaidi barani Afrika?

Soka Kenya; Gor Mahia bingwa

Klabu ya Gor Mahia ya Kenya imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka nchini humo kwa mara ya 21 sasa. Kikosi hicho cha Kocha Johnathan McKinstry, kilishuka dimbani Jumapili mjini Murang'a, eneo la Kati saa tisa mchana kuvaana na Muhoroni Youth ambapo iliitndika klabu hiyo inayoshushwa daraja mabao 3-0.

Ushindi huo umeifanya K'Ogali ifikishe pointi 67 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine za ligi hiyo inayoshirikisha klabu 18 zikiwamo. Mashabiki hawashikiki hawasemezeki.

Soka Tanzania; Azam yatinga fainali Shirikisho

Kwengineko, klabu ya Azam FC imetinga kwa fujo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) baada ya kuichapa Coastal Union mabao 3-0 kwenye mchezo wa nusu fainali uliopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.  Mabao yaliyoipeleka Azam FC fainali yalifungwa na Abdul Seleman 'Sopu' aliyepachika mawili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 42 baada ya mabeki wa Coastal Union kuunawa mpira wa shuti lililopigwa na Feisal Salum ndani ya eneo lao la hatari, na jingine kwa kichwa dakika ya 83 akiunganisha krosi ya Lusajo Mwaikenda. Jingine lilifungwa na Feisal Salum 'Fei Toto' dakika ya 73 kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona iliyochongwa na Sopu na kuwafanya mastaa hao wawili kuhusika kwenye mabao yote matatu. Azam FC imefuzu fainali hiyo kwa msimu wa pili mfululizo ambapo msimu uliopita ilipoteza kwenye fainali kwa bao 1-0 mbele ya Yanga katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Azam sasa itachuana na Yanga ambayo Jumapili iliitandika Ihefu bao 1 bila jibu. Goli la pekee la Stephane Aziz Ki limeipeleka Yanga fainali yake ya tano ya michuano ya CRDB Bank Federation Cup. Fainali ya msimu huu ya Kombe la Shirikisho itachezwa Juni 2.

Ligi ya EPL; City bingwa

Na hatimaye Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza ilifunga pazia lake la msimu huu siku ya Jumapili kwa kushuhudiwa mechi kadhaa za kusisimua. Klabu ya Manchester City imehifadhi taji hilo kwa mara ya nne mfululizo, baada ya kuichabanga West Ham mabao 3-1 katika mchezo wake wa mwisho uliopigwa Jumapili nyumbani Etihad. Phil Foden alicheka na nyavu mara 2, kabla ya Rodri kulizamisha kabisa jahazi la wageni.

La kufutia machozila West Ham lilifungwa na Mohammed Kudus. City sasa wameshinda taji hilo mara sita kati ya saba zilizopita kwenye Premier League.  City imemaliza ligi ikiwa na alama 91, pointi 2 zaidi ya hasimu wake wa karibu, klabu ya Arsenal, ambayo Jumapili hiyo ilijiongezea alama 3, baada ya kuizaba Everton mabao 2-1. Liverpool ambayo Jumapili iliinyoa bila maji Wolves kwa kuigaragazamabao 2-0, inafunga orodha ya tatu bora ikiwa na pointi 82.

……………..MWISHO..………….

 

 

Tags