Ulimwengu wa Michezo, Mei 27
(last modified Mon, 27 May 2024 07:14:20 GMT )
May 27, 2024 07:14 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Mei 27

Huu ni mukhtasari wa baadhi ya matukio makubwa ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika kona mbalimbali za dunia…..

Magongo: Iran bingwa wa Asia

Timu ya taifa ya mchezo wa magongo unaochezewa ukumbini ya Iran imetwaa ubingwa wa mashindano ya mabingwa wa Asia kwenye mchezo huo. Iran imetwaa taji hilo kwa mara ya tisa sasa baada ya kuibuka mshindi katika mchezo wa fainali dhidi ya Malaysia. Jamhuri ya Kiislamu imeibuka kidedea bada ya kuizaba Malaysia alama 7 kwa moja kwenye fainali hiyo.  

 

Mwanahoki wa Kiirani Amirmahdi Mirzakhani ametawazwa kuwa mfungaji bora wa mabao kwenye mashindano hayo ya magongo ya Asia baada ya kufunga jumla ya magoli 24. Pia ametangazwa kuwa mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi barani Asia. Iran na Malaysia zimejikatia tiketi za kushiriki fainali za Kombe la Dunia katika Mpira wa Magongo zitakazotifua mavumbi mwaka ujao nchini Croatia.

Iran yang'aa riadha walemavu

Iran imechota medali kochokocho kwenye Mashindano ya Dunia ya Riadha ya Walemavu yaliyofanyika nchini Japan. Yasin Khosravani aliipa Iran medali ya dhahabu katika mchezo wa kurusha chuma zito (shot put) kategoria ya F57. Alimaliza wa kwanza kwenye fainali ya safu hiyo baada ya kulirusha umbali wa mita 15.83. Raia wa Brazil Thiago Paulino dos Santos ameibuka wa pili huku raia wa Finland Teijo Koopikka akifunga orodha ya tatu bora. Wachezaji wengine wa Iran waliotwaa medali za dhahabu kwenye mashindano ya kimataifa ni Amirhossein Alipour kwenye mchezo wa kurusha kitufe, mtimkaji Hajar Safarzadeh, na mrusha mkuki Saeid Afrooz. Mashindano hayo ya World Para Athletics Championships 2024 yameandaliwa kama Kamati Ndogo ya Shirikisho la Riadha ya Walemavu Duniani (World Para Athletics), ambayo ipo chini ya Kamati ya Kimataifa ya Paralimpiki (International Paralympic Committee). Duru ya 11 ya mashindano hayo yalifanyika katika Uwanja Kobe Universiade Memorial mjini Kobe, Japan, kati ya Mei 17 na 25.

Wakati huo huo, Waziri wa Michezo wa Iran ametoa mwito wa kuharakisha mchakato wa kutekeleza kile kinachoitwa 'Usitishaji wa Olimpiki' (Olympic Ceasefire), ikiwa ni kampeni maalumu ya kulaani mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza. Kioumars Hashemi, Waziri wa Masuala ya Vijana na Michezo wa Iran alisema hayo Ijumaa katika hotuba aliyoitoa kwenye mkutano wa mawaziri wa michezo wa nchi wanachama Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai uliofanyika nchini Kazakhstan.

Alisema, "Kwa kuzingatia uhusiano wa karibu uliopo baina ya haki za binadamu na michezo, kwa kutilia maanani wajibu wa kimaadili wa mashirika na taasisi za michezo, napendekeza wanachama wa jumuiya ya SCO wapasishe maazimio ya kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina." Duru ya 33 ya Michezo ya Olimpiki ya Msimu wa Joto Kali inatazamiwa kufanyika Paris nchini Ufaransa baina ya Julai 26 na Agosti 11.

Ahly ya Misri mabingwa soka wa Afrika

Klabu ya Al Ahly ya Misri imefanikiwa kutwaa tena taji la Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Espérance Sportive de Tunis ya Tunisia katika mchezo wa marudiano ya fanali Jumamosi usiku wakiupigia nyumbani katika Uwanja wa Kimatafa wa Cairo katika mji mkuu wa nchi hiyo. Bao la pekee na la ushindi la Al Ahly alijifunga kiungo Mtogo, Roger Ben Boris Aholou dakika ya nne akijaribu kuokoa. Ikumbukwe kuwa, katika mechi ya mkondo wa kwanza, timu hizo zilitoa sare ya kutofungana mnamo Mei 18 katika Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi Jijini Radès nchini Tunisia.

 

Kwa kutwaa taji hilo la 12 la Ligi ya Mabingwa, Al Ahly watazawadiwa dola za Kimarekani Milioni 4, wakati Esperance watapata dola milion moja.

Katika hatua nyingine, klabu ya Coastal Union 'Wagosi wa Kaya' imejihakikisha nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao baada ya kukata tiketi ya CAF kwa kutoka suluhu na JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Kwa ushindi huo, sasa imefikisha pointi 42 ambazo haziwezi kufikiwa na KMC iliyokuwa ikiifukuzia na ambayo ina pointi 36, na hata kama itashinda mechi za mwisho itafikisha 39. KMC ilikuwa na uwezo wa kuzifikia pointi hizo 42, lakini kipigo cha wikendi kutoka kwa Simba kimeitibulia na kuiacha ibaki katika nafasi ya nne. Wekundu wa Msimbazi walipata ushindi laini wa bao moja bila jibu lililofungwa na Saidi Ntibazonkiza 'Saido'. Matokeo ya KMC yameirahisishia Coastal kukata tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao sambamba na vigogo, Simba, Yanga na Azam. Michuano hiyo ilikuja kuunganishwa na Kombe la CAF na kuzaliwa kwa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2004. Kwengineko, klabu ya Yanga imefanikwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ikiwa ni mara ya tatu mfululizo kuanzia msimu wa mwaka 2021/22 na imebakiwa na mechi tatu mkononi. Ubingwa huo ni wa 30 kwa Yanga katika historia yake, tangu ilipoanza kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 1968. Yanga ilionekana itakuwa mabingwa wa msimu huu mapema kuanzia Oktoba 23, mwaka jana ilipoichapa Azam FC mabao 3-2, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam licha ya kufungwa katika mechi ya marudiano iliyofanyika Machi 17, mwaka huu. Baada ya Yanga kugawana pointi tatu na Azam, ikachukua pointi zote sita kutoka kwa watani wao Simba, hivyo ikawa imekusanya pointi tisa kati ya 12, kutoka kwa wapinzani wake wanaoonekana kutaka ubingwa huo.

Riadha: Kenya yawika tena

Mwanariadha nyota wa Kenya, Beatrice Chebet ameweka rekodi ya dunia mbio za mita 10,000 baada ya kushinda Eugene Diamond League nchini Amerika kwa dakika 28:54.14, Jumamosi. Alifuta rekodi ya raia wa Ethiopia Letesenbet Gidey aliyetimka umbali huo kwa dakika 29:01.03 mjini Hengelo, Uholanzi mnamo Juni 8, 2021. Chebet, ambaye ni bingwa wa mbio za nyika duniani, ameimarisha muda wake bora kutoka dakika 33:29 aliotimka Machi 2020 ugani Kasarani jijini Nairobi hadi 28:54.14. Alifuatwa kwa karibu na raia wa Ethiopia Gudaf Tsegay (29:05.92) na Wakenya Lilian Kasait (29:26.89) na Margaret Chelimo (29:27.59) ambao walipata muda bora kila mmoja. Bingwa huyo wa mbio za mita 5,000 za Jumuiya ya Madola na Afrika, ambaye pia ni mshikilizi wa rekodi ya dunia mbio za kilomita tano barabarani, pia amefuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki jijini Paris, Ufaransa mnamo Julai 26 hadi Agosti 14. Mbio hizo zilivutia washiriki 21 wakiwemo Wakenya 15.

Dondoo za Hapa na Pale

Klabu ya Manchester United imepunguza mwanya wa mataji ya Kombe la FA kati yake na mahasimu Arsenal baada ya kuivua ubingwa Manchester City kwa kuichapa 2-1 kwenye fainali ya Kombe la FA ugani Wembley, Jumamosi jioni. United, ambayo itashiriki Europa baada ya ushindi huo muhimu, ina mataji 13 ya dimba hili, moja nyuma ya Arsenal inayoshikilia rekodi. Ililipiza kisasi dhidi ya City kupitia mabao ya chipukizi Alejandro Garnacho na Kobbie Mainoo. City, ilibwaga United 2-1 katika fainali mwaka 2023, na katika fainali ya Jumamosi, wachezaji wake walipoteza nafasi nzuri. Phil Foden na Erling Haaland walipoteza nafasi za wazi.

Image Caption

 

Kocha Erik ten Hag amekuwa akikabiliwa na presha ya kufukuzwa kwa sababu ya msimu duni ambapo United ilimaliza Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika nafasi ya nane. Mashetani Wekundu wa United sasa wamelemea City mara sita katika mechi nane za FA wamekutana. Mbali na hayo ufunguzi wa Mashindano ya Afrika ya mpira wa miguu kwa vijana chini ya umri wa miaka 15 ‘African Schools Football Championship 2024’ ulifanyika katika Uwanja wa New Amaan Complex, kisiwani Unguja, Zanzibar. Timu ya Wasichana ya Tanzania imeanza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Morocco katika Kundi A. Kundi B, Wasichana wa Taifa la Togo wametoshana nguvu kwa suluhu tasa ya 0-0 dhidi ya Gambia, ilhali kundi hilohilo Afrika Kusini wametoka sare ya 1-1 dhidi ya Uganda. Upande wa wavulana, Kundi A, Tanzania wametoka suluhu ya 0-0 dhidi ya Senegal. Kundi B, Guinea wamegawa kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Benin wakati wavulana wa Afrika Kusini wameibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Libya. Tanzania ni bingwa mtetezi na mwenyeji wa michuano hiyo inayoendelea.

Huku hayo yakarifiwa, Barcelona ilimtimua kocha Xavi Hernandez siku ya Ijumaa baada ya miamba hao wa Catalan kushindwa kushinda kombe msimu huu lakini wiki chache tu tangu yeye na rais wa klabu Joan Laporta wakubali kusalia kwenye wadhifa huo. Aidha Thiago Motta anatazamiwa kusaini mkataba wa miaka mitatu na Juventus katika siku zijazo, kwa mujibu wa Tuttomercatoweb. Na Stefano Pioli amefukuzwa kazi kama kocha mkuu wa AC Milan miaka miwili baada ya kuwaongoza kutwaa ubingwa wa Serie A, miamba hao wa Italia walitangaza Ijumaa. AC Milan ilisema katika taarifa kwamba Pioli, ambaye alikuwa chini ya mkataba hadi 2025, “ataondoka baada ya kumalizika kwa msimu huu, baada ya kuinoa Kikosi cha Kwanza tangu Oktoba 2019”.

………………TAMATI…………..

 

 

 

 

 

Tags