Jul 08, 2024 07:22 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Jul 8

Natumai u mzima wa afya mpenzi msikilizaji, na karibu tuangazie japo kwa mukhtasari baadhi ya matukio makubwa yaliyoshuhudiwa viwanjani ndani ya siku saba zilizopita katika kona mbalimbali za dunia.....

Iran bingwa wa kutunisha misuli Asia

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka kidedea kwenye Mashindano ya Asia ya Utunishaji Misuli ya 2024. Iran siku ya Jumapili ilitawazwa bingwa wa mashindano hayo ya IFBB Asian Championships yaliyofanyika mjini Ulaanbaatar, Mongolia, baada ya kuzoa medali 14 za dhahabu, 6 za fedha na 4 za shaba.

Image Caption

Snuka: Iran ya tatu Asia

Iran imeibuka ya tatu kwenye Mashindano ya Asia ya ACBS ya 2024 kwenye mchezo wa snuka yaliyofanyika nchini Saudi Arabia. Wairani Amir Sarkhosh, Ali Gharagozlou, na Arman Dinarvand wamemaliza katika nafasi ya tatu kwenye mchezo huo wa kugonga tufe mezani, baadaya ya kuzidiwa kete na Thailand.  Wanamichezo zaidi ya 200 wa kike na kiume kutoka nchi 15 za Asia wameshiriki mashindano hayo yaliyofunga pazia lake Julai 5 huko Saudia.

Riadha: Olimpiki

Takriban wiki tatu kabla ya kuanza Michezo ya Olimpiki ya 2024 jijini Paris, Ufaransa, Iran imeteua wanamichezo 40 watakaoiwakilisha Jamhuri ya Kiislamu kwenye mashindano hayo ya kimataifa.

Kamati ya Olimpiki ya Iran imeteua wanariadha 29 wa kiume na 11 wa kike watakaoshiriki kwenye michezo mbalimbali kama mieleka, unyanyuaji vyuma vizito, tenisi ya mezani, uendeshaji baiskeli, ukweaji, uogoleaji. Vitara, taekwondo miongoni mwa michezo mingine.

 

Riadha: Mkenya avunja rekodi

Nyota wa mbio za mita 1,500 za dunia na Olimpiki, Mkenya Faith Kipyegon anaendelea kumiminiwa sifa baada ya kuvunja rekodi yake ya dunia katika kwenye duru ya nane ya Ligi ya Almasi (Diamond League) huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa, siku ya Jumapili. Kipyegon ameshinda taji hilo kwa kutumia dakika 3, sekunde 49.04, akifuta rekodi ya dakika 3, sekunde 49.11 aliyoweka mjini Florence nchini Italia mwaka jana. Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 30 anasalia mwanamke wa kwanza kukamilisha 1,500m chini ya dakika 3, dakika 50.00.

Kipyegon alifuatwa kwa karibu na Jessica Hull kutoka Australia (3:50.83), Muingereza Laura Muir (3:53.79), Linden Hall kutoka Australia (3:56.40), Muingereza Georgia Bell (3:56.54) na Mkenya Susan Ejore (3:57.26), mtawalia. Jacob Krop alitawala mbio za mita 3,000 kwa kutumia dakika 7, sekunde 28.83, naye mshikilizi wa rekodi ya dunia mbio za 3,000 kuruka viunzi na maji, Beatrice Chepkoech akasikitisha katika nafasi ya tisa. Emmanuel Wanyonyi aliyejivunia muda bora mwaka huu baada ya kukamilisha 800m kwa dakika 1:41.70 ugani Nyayo jijini Nairobi mnamo Juni 15 akifuzu Olimpiki, aliridhika na nafasi ya pili kwa muda wake mpya bora wa 1:41.58.

Djamel Sedjati kutoka Algeria alitwaa taji la Paris Diamond League kwa muda mpya bora dunia mwaka huu wa 1:41.56. Sedjati alikosa rekodi ya Paris Diamond League ya Mkenya David Rudisha kwa sekunde 0.02. Alikuwa na muda bora wa 1:43.06. Mfaransa Gabriel Tual (1:41.61) na Wakenya Aaron Cheminingwa (1:42.08) na bingwa wa zamani wa Jumuiya ya Madola Wyclife Kinyamal (1:42.08) walifunga mduara wa tano-bora kutoka orodha ya washiriki 12. Mshindi wa medali ya fedha kwenye Michezo ya Afrika Amos Serem na bingwa wa Jumuiya ya Madola Abraham Kibiwott nao waliridhika na nafasi ya pili na tatu kwa dakika 8:02.36 na 8:06.70 katika 3,000m kuruka viunzi na maji. Walimaliza nyuma ya Muethiopia Abrham Sime (8:02.36).

Droo ya kuelekea AFCON 2025

Droo ya kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 ambazo zitafanyika Morocco imechezeshwa Julai 4 jijini Johannesburg, Afrika Kusini, ambapo timu za nchi 48 zimebaini wapinzani wao kwenye hatua ya makundi kwenye duru ya 35 ya michuano hiyo, inayofanyika kila baada ya miaka miwili. Timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' imepangwa Kundi H na DRC, Ethiopia na Guinea; huku Kenya, mwakilishi mwingine wa Afrika Mashariki akipangwa kwenye Kundi J pamoja na Cameroon, Namibia, na Zimbabwe.

Kundi K inazileta pamoja Afrika Kusini, Uganda, Jamhuri ya Congo, na Sudan Kusini. Wenyeji wa michuano hiyo, Morocco wamepangwa Kundi B pamoja na Gabon, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Lesotho. Hatua hiyo ya makundi kuwania kufuzu Afcon 2025 zitaanza kuchezwa Septemba mwaka huu. Jumla ya timu 24 zitafuzu kucheza fainali hizo, ambapo bingwa mtetezi ni Ivory Coast.

Dondoo za Hapa na Pale

Wanamieleka wa Russia ambao walipewa idhini ya kushiriki katika Michezo ya Olimpiki wamekataa mwaliko wa kushiriki mashindano hayo ya msimu wa joto kali mjini Paris, Ufaransa. Shirikisho la Olimpiki la Russia limesema wanamieleka 10 wa nchi hiyo waliofuzu vigezo vilivyowekwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) na kuruhusiwa kushiriki mashindano hayo ya kimataifa, wametangaza kususia michezo hiyo, wakilalamikia vikwazo na vizingiti vya IOC. Awali, IOC ilikuwa imewazuia wanamieleka hao pamoja na wanamichezo wengine wa Russia kushiriki Michezo ya Olimpiki kutokana na operesheni ya kijeshi ya Moscow huko Ukraine. OIC baadaye iliwaruhusu wanamichezo kadhaa wa Russia washiriki mashindano hayo lakini kwa masharti mazito, lakini sasa wanamieleka hao 10 wamesusia mwaliko huo.

Na baada ya Uhispania na Ufaransa kutangulia nusu fainali za Kombe la Mataifa ya Ulaya (EURO2024) zinazofanyika Ujerumani, Uingereza pia imesogea mbele lakini kwa mbinde. England hiyo imetinga nusu fainali ya Euro 2024 kwa kuwatoa Uswisi kwenye upigaj matuta. Iliibamiza Uswisi mikwaju 5 ya penati kwa 4. Hii ni baada ya kutoshana nguvu na kutoa sare ya bao 1-1 katika dakika za ada na nyongeza.

Uholanzi pia wametinga nusu fainali ya Euro kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 20. Hii ni baada ya kuicharaza Uturuki mabao 2-1. Ufaransa walitangulia kwenye meza hiyo ya wakubwa, baada ya kuizaba Ureno kwenye mikwaju ya penati kwa kuitandika mabao 5-4. Waliingia upigaji matuta baada ya kutoa sare tasa. Ufaransa itawajihiana na Uhispania kwenye nusu fainali ya kukata na shoka siku ya Jumanne katika Uwanja wa Allianz Arena mjini Munich. Siku inayofuata, Uingereza itatoana jasho na Uholanzi katika Uwanja wa Singal Iduna Park.

………………MWISHO.…………..

 

 

Tags