Aug 19, 2024 06:24 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Agosti 19

Natumai hujambo mpenzi msikilizaji na hususan shabiki na mfuatiliaji wa habari za spoti. Karibu tuangazie japo kwa mukhtasari baadhi ya matukio makubwa ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita kote duniani…

Ligi Kuu ya Soka ya Iran

Ligi Kuu ya Soka ya Iran imeanza kuroroma na kutifua mavumbi katika viwanja, miji na mikoa mbali mbali ya Jamhuri ya Kiislamu. Klabu ya Esteghlal imeanza vyema ligi, japo kwa mbinde, baada ya kuambulia bao moja bila jibu ilipochuana na Shams Azar Ijumaa usiku katika mechi yake ya wiki ya kwanza ya ligi ya Iran inayofahamika pia kama Ligi ya Wataalamu wa Ghuba ya Uajemi.

Bao la ushindi la The Blue ya Tehran lililopasishwa na mfumo wa video ya refa msaidizi VAR lilipachikwa wavuni katika dakika za lala salama na Mohammadhossein Eslami katika mechi ambayo Esteqlal iliishia kushinda mabao 2-1.

Huko mjini Isfahan, klabu ya Sepahan ilimshukia mwanagenzi Chadormalu mabao 3-1, ambayo ndo kwanza inakula kwenye meza ya wakubwa. Watengeneza matrekta waliibamiza Mes mabao 2-0 huko Kerman, wakati ambapo Havadar ilishindwa kutamba hapa Tehran ilipovaana na Kheybar ambayo pia imepandishwa hadhi majuzi. Siku ya Alkhamisi, mabingwa watetezi, klabu ya Persepolis ililazimishwa sare ya bao 1-1 iliposhuka dimbani kuvaana na Zob Ahan.

Chumba cha VAR katika Ligi ya Iran

Na ni kudokeza tu kwamba, Shirikisiho la Soka Duniani FIFA limeidhinisha matumizi ya mfumo wa video wa VAR kwenye ligi ya soka ya Iran iliyong'oa nanga Agosti 15.

Soka Afrika; Yanga yaanza vizuri

Klabu ya Yanga SC ya Tanzania imeibuka na ushindi mnono katika mchezo wao wa kwanza katika hatua za awali za michuano ya Klabu Bingwa Afrika. Hii ni baada ya kuigaragaza klabu ya Vital’O FC ya Burundi magoli manne kwa nunge katika dimba la Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam. Magoli ya Wananchi katika mechi hiyo ya CAF yalifungwa na Prince Dube, Cleopas Chama, Clement Mzize na Stephane Aziz Ki.

Wachezaji wa Yanga wakishangilia goli

Kwa ushindi huo, mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga walikabidhiwa kitita cha Sh. milioni 20, kila goli likiwa na thamani ya Sh. milioni tano, ambazo zitakuwa zinatolewa katika kila mechi ya kimataifa na Rais, Samia Suluhu Hassan. Yanga iliwaadhibu Warundi hao katika hali ambayo, Vital’O FC ndiyo timu yenye historia kubwa nchini Burundi baada ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka wa 1992 ikiwa na Makombe 21 ya Ligi Kuu Burundi. Mshindi wa jumla wa mechi ya Yanga dhidi ya Vital'O, anatazami wa kukutana na mshindi kati ya CBE ya Ethiopia au SC Villa ya Uganda.

Huku hayo yakiarifiwa, Azam iliyomaliza ya pili katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Jumapili iliambulia ushindi mwembamba wa bao 1-0 wakati ikiupigia nyumbani katika Uwanja wa Azam Complex dhidi ya APR ya Rwanda. JKU ya Zanzibar iligeuzwa kichwa cha mwendawazimu ilipovaana na Waarabu wa Pyramids ya Misri katika dimba la Juni 30 na kupewa kichapo cha mbwa cha mabao 6-0.

Michuano ya Klabu Bingwa Afrika huandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika CAF

Kadhalika baada ya miaka 35, kwa mara ya kwanza klabu ya Coastal Union ya Tanzania ilishuka uwanjani wikendi kucheza Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, Bravos do Maquis ya Angola. Kwa ufupi wawakilishi hao wa Tanzania, wameanza vibaya kwa kugaragazwa mabao 3-0.

Wakati huo huo, klabu ya Polisi ya Kenya imeanza mashindano hayo ya kikanda kwa sare tasa ilipovaana na klabu ya Kahawa ya Ethiopia Jumapili katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi. Kocha wa maafande hao wa Kenya, Anthony Kimani anasema bado ni mapema mno kuihukumu timu yake, na kwamba wana matumaini ya kusogea mbele.

Mwakilshi mwingine wa Kenya kwenye mashindano hayo, klabu ya Gor Mahia siku ya Jumapili ikiupigia ugenini jijini Juba ilipokezwa kichapo laini cha bao 1 bila jibu na klabu ya Al-Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini.

Ligi ya EPL yarejea kwa kishindo

Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza imerejea kwa kishindo huku miamba ya kandanda katika nchi hiyo ya Ulaya ikianza vizuri mashindano hayo ya mpira wa miguu yanayotazamwa zaidi duniani. Bao la dakika ya lala salama yake mshambuliaji mpya wa Manchester United, Joshua Zirkzee liliwapa Mashetani Wekundi ushindi muhimu dhidi ya Fulham Ijumaa usiku. Arsenal pia imeanza vyema msimu, kwa kuisasambua Wolves mabao 2-0. Mabao ya Wabeba Bunduki wakichezea nyumbani Emirates, yalifungwa na Kai Havertz na Bukayo Saka.

Klabu ya Manchester City Jumapili iliitandika Chelsea ambayo ilikuwa ikipugia nyumbani Stamford Bridge mabao 2-0 yaliyotiwa kimyani na Erling Halaand Mateo Kovacic.

Liverpool pia imeitandika Ipswich Town mabao 2-0 katika mchezo wao wa ufunguzi, wakati New Castle ilipokuwa ikiuzaba Southampton bao 1-0. Nikudokeze kuwa, Ligi ya Uhispania 'La Liga' pia imeanza kwa kishindo, huku Ligi Kuu ya Ujerumani 'Bundesliga' ikitazamiwa kuanza Agosti 23.

………………..MWISHO…………..

 

 

 

Tags