Ulimwengu wa Michezo, Agosti 31
Natumai u bukheri wa afya hapo ulipo msikilizaji mpenzi. Karibu tuangazie baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbali mbali za dunia.
CAFA: Iran yaizaba Afghanistan
Timu ya taifa ya soka ya Iran imeanza michuano ya kikanda ya CAFA kwa mguu wa kulia. Hii ni baada ya wanakandanda wa timu hiyo ya Jamhuri ya Kiislamu kutoka nyuma na kuibinjua Afghanistan mabao 3-1 katika mechi ya ufunguzi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Asia ya Kati (CAFA) 2025 siku ya Ijumaa. Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Hisor Central mjini Hisor, Tajikistan, Omid Mousavi aliifungia Afghanistan bao la kuongoza dakika ya 21, lakini Majid Aliyari alisawazisha dakika tano baadaye. Amirhossein Hosseinzadeh alifanya mambo kuwa 2-1 katika dakika ya 36 huku Aliyari akicheka na nyavu kwa mara nyingine kunako dakika ya 64.

Iran imemenyana na India Septemba Mosi, na sasa inatazamiwa kushuka dimbani kutoana udhia na Tajikistan Septemba 4, katika mechi za Kundi B. Kundi A linajumuisha Uzbekistan, Kyrgyzstan, Turkmenistan na Oman.
Iran bingwa ulengaji shabaha
Kwa mara ya kwanza kabisa timu ya walengaji shabaha ya Iran imeweka historia katika Mashindano ya 16 ya Shabaha ya Asia, kwa kujinyakulia medali ya dhahabu ya mtu binafsi na kwa timu, kwa kuyatua risasi umbali wa mita 50 kwa kutumia bastola. Javad Foroughi alionyesha mchezo wa wa kiwango bora, akishinda pointi 554 na kupata medali ya kwanza ya dhahabu ya Iran katika kategoria ya mita 50. Muirani mwenzake Amir Johari Kho alifuata kwa karibu na pointi 551, na kupata medali ya fedha. Vahid Golkhandan, mshindani wa tatu wa Iran, alimaliza wa tano kwa alama 547, akikamilisha orodha la kikosi cha kitaifa kilichong'ara. Watatu hao, Foroughi, Johari Kho, na Golkhandan, waliunganisha vikosi na kujikusanyia pointi 1652, na kuipeleka Timu ya Iran kileleni mwa jukwaa katika safu ya timu. India na Korea Kusini zilitwaa nafasi ya pili na ya tatu mtawalia.
CHAN tamati; Morocco yailaza Madagascar
Ndoto ya Madagascar ya kutwaa kwa mara ya kwanza Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) ilizimwa na mabingwa watetezi Morocco, ambao siku ya Jumamosi walikuwa na kibarua kigumu cha kupambana na timu ya taifa ya soka ya kisiwa hicho cha kusini mashariki mwa Afrika. Simba wa Atlas walishinda taji lao la tatu la CHAN baada ya kutoka nyuma na kuiduwaza Madagascar kwa kuichabanga mabao 3-2 katika mechi ya kusisimua iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kasarani jijini Nairobi. Nyota wa Mechi Oussama Lamlioui alifunga mabao mawili, ikiwa ni pamoja na bao lililowapa ushindi Waarabu hao wa Kaskazini mwa Afrika. Lamlioui ametawazwa kuwa Mfungaji Bora wa Puma wa Michuano ya CAF ya Mataifa ya Afrika (CHAN) baada ya kufunga bao lake la tano na la sita katika mechi hiyo katika ushindi wa mabao 3-2 wa Atlas Lions dhidi ya Madagascar kwenye fainali ya kukata na shoka Jumamosi. Ushindi huo unaifanya Morocco kuongeza mataji yao ya CHAN hadi matatu, kwani walishinda mwaka 2018 na 2020, na kuwafanya kuwa taifa lenye mafanikio makubwa katika historia ya mashindano hayo ya soka ya bara Afrika, kwa wachezaji wanaoshiriki ligi za ndani barani humo. Rais William Ruto wa Kenya ambaye aliikabidhi Morocco kombe hilo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mahamoud Ali Yousuf, Rais wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA, Gianni Infantino na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika CAF, Patrice Motsepe ambao walikuwa ugani Kasarani wakati wa fainali hiyo, wamewapongeza vijana hao wa Kiarabu kwa kuibuka kidedea.

Senegal iliibuka mshindi wa tatu kwenye michuano hiyo ya kibara, baada ya kuitandika Sudan mabao 4-2 kupitia mikwaju ya penalti, kufuatia sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Kitaifa wa Mandela jijini Kampala siku ya Ijumaa. Mabingwa hao watetezi, walitolewa tonge mdomoni na kutofika fainali baada ya kushindwa na Morocco kwa mikwaju ya penalti katika nusu fainali, walionyesha uthabiti kwa mara nyingine katika mechi iliyokuwa na ushindanii mkali, ya kuwani medali ya shaba. Morocco wameondoka na kitita cha dola milioni 3.5 za Marekani kwa ushindi huo wa CHAN, huku Madagascar wakituzwa Dola milioni 1.2. Mshindi wa tatu, Senegal kwa upande wao amezawadiwa dola laki 7. Safari ya Taifa Stars ya Tanzania, Harambee Stars ya Kenya na Cranes ya Uganda kwenye michuano hiyo ya kibara iliishia kwenye hatua ya robo fainali baada ya timu hizo za Afrika kukubali kipigo kutoka kwa Morocco, Madagascar na Senegal kwa usanjari huo. Hata hivyo, Kenya, Tanzania na Uganda, wenyeji wa michuano ya CHAN waliyaaga mashindano hayo kiume, baada ya kuondolewa kwenye robofainali, na sasa wanajinoa kwa ajili ya michuano ijayo ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia la kipute cha AFCON.
Dondoo za Hapa na Pale
Miamba ya soka nchini Tanzania klabu za Yanga na Simba zitavaana Desemba 13, 2025 katika mchezo wa duru ya kwanza la Ligi Kuu ya Tanzania Bara, mchezo utakaopigwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga akiwa mwenyeji. Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu nchini humo (TPLB), mchezo huo utaanza saa 11 jioni na kwamba mchezo wa marudiano utafanyika Aprili 4, mwakani 2026.

Kabla ya hapo, timu hizo mbili zinatazamiwa kuvaana katika mchezo wa Ngao ya Jamii, mechi inayotajwa kuwa ya kisasi na heshima mnamo Septemba 16 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Mchuano huwa wa kuashiria kuanza kwa ligi, unasubiriwa kwa hamu na shauku kuu na mashabiki kindakindaki wa watani hawa wa jadi.
Huku hayo yakiarifiwa, michuano ya Kombe la Cecafa Kagame Cup itatoa muendelezo mwafaka kwa Ligi ya Mabingwa ya CAF, itakayopangwa Septemba 2-15 jijini Dar es Salaam, Tanzania. Mashindano hayo ya kanda ya klabu 12 yataleta pamoja timu za juu kutoka Afrika Mashariki na Kati ili kuwania tuzo hiyo. Kenya Police, mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya 2024/2025, wataongoza kampeni ya nchi hiyo katika Kundi A pamoja na Singida FC ya Tanzania, Garde Côte ya Djibouti na Ethiopia Coffee. Kundi B litakuwa na APR ya Rwanda, NEC ya Uganda, Bumamuru ya Burundi na Mlandege ya Zanzibar, huku Kundi C likiwakutanisha Al Hilal Omdurman ya Sudan na Al Ahly SC Wad Madani, Kator ya Sudan Kusini na Mogadishu City kutoka Somalia. Katibu Mkuu wa CECAFA Auka Gacheo amekaribisha mpango mpango wa kujitokeza wafadhili wapya, akisema, "Rais wa Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame alikuwa mfadhili wa awali wa Kombe la Kagame, na sasa tuna wafadhili wapya. Ni mwanzo mzuri. Udhamini unaongeza thamani, na ninatumai klabu zitafurahia."

Na Jose Mourinho amebwaga manyanga kama meneja wa klabu ya Fenerbahce ya Uturuki, baada ya zaidi ya mwaka mmoja. Kuondoka kwa Mreno huyo kumekuja siku mbili baada ya klabu hiyo ya Istanbul kuondolewa katika mchujo wa Ligi ya Mabingwa na Benfica. Katika taarifa, Fenerbahce ilisema Mourinho "aliachana" na klabu hiyo, kabla ya kumshukuru mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 62 kwa juhudi zake. "Tunamtakia mafanikio katika maisha yake ya baadaye," taarifa hiyo iliongeza. Mourinho, ambaye ameongoza klabu 10 zikiwemo Chelsea, Manchester United na Tottenham, aliiongoza Fenerbahce hadi nafasi ya pili kwenye ligi, wakati wa msimu pekee wa kuinoa klabu hiyo, lakini muda wake ulikumbwa na utata.
……………….TAMATI…………….