Ulimwengu wa Spoti, Sep 22
Natumai u mzima wa afya mpenzi msikilizaji popote pale ulipo. Ufuatao ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbali mbali za dunia.
Futsal Asia; Iran yaanza vizuri
Iran ambao ni mabingwa watetezi imeanza kampeni yao ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Futsal la Asian zitakazopigwa Indonesia 2026, kwa ushindi wa mabao 12-0 dhidi ya Bangladesh katika mchezo wa Kundi G uliopigwa Jumamosi.

Bangladesh ilitoa upinzani mkali kwa Iran ambao ni mabingwa mara 13 wa futsal hapa Asia, lakini juhudi zao hazikuwazuia wachezaji wa Iran wakose kucheka na nyavu mara chungu nzima. Nyota wa mchezo huo wa wikendi alikuwa Hossein Tayebi aliyefunga mabao matatu ya hattrick.
Handiboli: Iran yainyuka Qatar
Iran ilichabanga Qatar 46-25 katika Duru ya Kwanza ya Mashindano ya Mpira wa Mikono ya Wanaume weye chini ya miaka 17 ya Asia Jumamosi. Ushindi huo unakuwa ushindi wa sita wa Iran katika kampeni hiyo, kwani mabarobaro hao wa Kiajemi hapo awali walikuwa wamezinyoa kwa chupa Maldives, Syria, Korea Kusini, Kuwait na Jordan. Timu hiyo ya Iran sasa imejikatia tiketi ya nusu fainali na inatazamiwa kushika dimbani kuvaana na Bahrain siku ya Jumanne. Korea Kusini pia itacheza na Qatar katika nusu fainali nyingine.
Wanamieleka wa Iran wapokewa kifalme
Timu ya taifa ya Iran ya mchezo wa mieleka aina ya freestyle, baada ya kuibuka kidedea kwenye Mashindano ya Dunia ya Mieleka ya 2025 huko Zagreb, Croatia, ilirejea nyumbani na kupokewa kishujaa na kifalme kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Imam Khomeini hapa jijini Tehran siku ya Ijumaa. Wananchi wa Iran walipowapokea kwa mbwembwe za aina yake mabingwa hao wa dunia. Jumatatu ya wiki iliyopita, timu hiyo ya taifa ya mieleka ya kujiachia ya Iran ilitwaa taji la ubingwa katika Mashindano ya Dunia ya Mieleka huko Zagreb, Croatia, huo ukiwa ushindi wao wa kwanza baada ya kupita miaka 12. Timu hiyo ilimaliza mashindano hayo ikiwa na medali mbili za dhahabu, mbili za fedha na tatu za shaba, na jumla ya alama 145, ikiiacha nyuma timu ya mieleka ya Marekani.

Haya yanajiri huku wenzao wa mieleka aina ya Greco-Roman ikifanya vyema pia katika mashindano hayo ya dunia huko Zagreb. Timu hiyo ya mieleka ya Greco-Roman ya Iran ambayo imewahi kutwaa ubingwa tena mwaka 1961, 1965, 1998, 2002, na 2013, siku ya Jumapili ilivikwa taji baada ya kuzoa medali kochokocho zikiwemo za dhahabu kwenye mashindano hayo ya kimataifa nchini Croatia. Baadhi ya wanamieleka wa Jamhuri ya Kiislamu walioshinda medali za dhahabu ni pamoja na Gholamreza Farrokhi katika safu ya kilo 82, Amin Mirzazadeh kwenye kategoria ya kilo huku Mohammadhadi Saravi akihitimisha ukame wa miaka minne wa kutoshinda taji la dunia. Hi ni baada ya kumchakaza Artur Sargsyan wa Armeni kwa alama 3-1 katika fainali ya wanamieleka wenye kilo 97 Jumamosi usiku. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amezipongeza timu hizo za taifa za Iran kwa kung'ara katika Mashindano ya Mieleka ya Dunia ya 2025 yaliyofanyika mjini Zagreb, Croatia.

Katika ujumbe wake wa tahania, Imam Khamenei amepongeza kujitolea kunakostaajabisha na mwenendo wa kustahiki pongezi kubwa ulioonyeshwa na mabingwa hao wa mieleka ya freestyle na Greco Roman. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Natoa shukrani zangu kwa timu ya mieleka, mabingwa wa dunia kwa juhudi zao za kustaajabisha na mwenendo wao wa kupendezesha. Mchanganyiko wa nguvu na umaanawi hujenga tunu adhimu. Nakupeni heko!"
Wanariadha wa Kenya wang'ara Tokyo
Wanariadha wa Kenya wameiheshimisha si tu kanda ya Afrika Mashariki, bali bara zima la Afrika kwa kung'ara katika Mashindano ya Dunia ya Riadha ya Tokyo nchini Japan. Hii ni baada ya kuibuka mshindi wa pili kwenye jedwali la medali katika mashindano hayo ya kimataifa nyuma ya Marekani, baada ya kuzoa jumla ya medali 11 zikiwemo 7 za dhahabu. Beatrice Chebet na Faith Kipyegon walishinda dhahabu na fedha mtawalia katika mbio za mita 5,000 kwa wanawake. Chebet aliwatifulia mavumbi Nadia Battocletti wa Italia, na Gudaf Tsegay wa Ethiopia kushinda medali yake ya pili ya dhahabu mjini Tokyo, kwa kutumia dakika 14:54.36, Kipyegon alimaliza kwa kutumia dakika 14:55.07, huku Battocletti akirekodi muda wa 14:55.42.

Wakati huo huo, Mkenya Emmanuel Wanyonyi ameshinda medali ya dhahabu katika mbio za mita 800 kwa wanaume katika Riadha za Dunia za 2025 na kumshinda bingwa mtetezi Marco Arop, aliyetumia dakika 1:41.95 na kumaliza wa tatu, huku Djamel Sedjati aliyeshinda medali ya shaba kwenye Olimpiki, akitwaa medali ya fedha. Katika mbio hizo za mita 800 safu ya wanawake, mwanadada anayeibukia kwa kasi wa Kenya, Lilian Odira aliibuka kidedea kwa kutumia dakika moja, sekunde 54.68 na kuifanya bendera ya Kenya iendelee kupepea katika riadha za kimataifa.
Tukisalia katika riadha, Kenya imeendelea kuithibitishia dunia kuwa ni moto wa kutea mbali katika mbio za masafa marefu. Hii ni baada ya wanariadha wake kuibuka washindi katika duru ya 51 ya Berlin Marathon kwa upande wa wanaume na wanawake, ingawa wameshindwa kuvunja rekodi ya dunia. Mwanariadha Sabastian Sawe mwenye umri wa miaka 29 alishinda mbio za wanaume kwa muda wa saa 2:02:15, ikiwa ni miezi mitano tangu kushinda London Marathon. Kwa upande wa wanawake, Rosemary Wanjiru aliibuka mshindi baada ya kuongoza kuanzia kilomita 25.
Ngao ya Jamii; Yanga yatamba
Klabu ya Yanga SC ya Tanzania ilivuna ushindi laini wa bao 1-0 dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC, katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliotandazwa Septemba 16 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam. Mchezo huo uliokuwa wa ushindani mkubwa ulivutia maelfu ya mashabiki kutoka pande zote mbili, huku kila timu ikionyesha kiwango cha juu cha maandalizi kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.

Bao pekee katika mchezo huo lilifungwa katika dakika ya 57 ya mchezo na mshambuliaji hatari wa Yanga, Pacome Zouzoua, goli ambalo liliamsha shangwe kubwa kwa mashabiki wa Yanga waliokuwa wamejazana kwa wingi uwanjani. Mchezo huu wa Ngao ya Jamii hutumika kama utangulizi rasmi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, na ushindi huu unaipa Yanga SC hamasa kubwa kuelekea kampeni za msimu wa 2025/2026.
Wakati huo huo, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, wameanza kwa kishindo katika hatua za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3 – 0 dhidi ya Wiliete SC ya Angola katika mchezo uliopigwa Ijumaa ya Septemba 19, kwenye Uwanja wa Estádio 11 de Novembro (Novemba 11), nchini Angola. Yanga wamerejea nyumbani kujiandaa kwa mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki ijayo katika dimba la Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam. Nao Maafande wa Kenya siku ya Jumamosi waliibamiza Mogadishu City ya Somalia mabao 3-1 katika mchuano wao wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa ya CAF uliopigwa katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi. Kenya Police na Mogadishu City zitavaana katika mechi ya marudiano Jumapili ijayo jijini Nairobi. Washabiki wa Mogadishu wanasisitiza kuwa watashinda mechi ijayo ambayo itapigiwa huko huko jijini Nairobi.
Dondoo za Hapa na Pale
Timu ya taifa ya soka ya wanawake wenye chini ya miaka 20 ya Kenya "Rising Starlets", imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Ethiopia katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA la U20 la 2026. Kwenye mchezo huo uliopigwa Jumapili katika Uwanja wa Abebe Bikila mjini Addis Ababa, Starlets walikuwa wa kwanza kuona lango la wenyeji, huku wakipoteza fursa nyingi za kuongeza mabao. Wenyeji walijitutumua na kufanya mambo kuwa sawa bin sawa. Mkufunzi wa Kenya, Jackline Juma anaeleza kuwa watarekebisha mapungufu yaliyojitokeza. Mechi ya marudiano itachezwa Septemba 28 katika uwanja wa Ulinzi Sports Complex, jijini Nairobi.

Na Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sánchez ametoa wito wa kutojumuishwa utawala wa kizayuni wa Israel katika mashindano ya kimataifa ya michezo kutokana na vita na jinai zake huko Gaza. Pedro Sánchez amewaambia Wabunge wa Chama chake cha Kisoshalisti kwamba, "Israel haiwezi kuendelea kutumia jukwaa lolote la kimataifa kusafisha sura yake." Amesisitiza kuwa, Israel inapaswa kutengwa kutokana na jinai zake inazofanya dhidi ya Wapalestina hususan katika Ukanda wa Gaza. Hivi karibuni pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania aliunga mkono wito wa kuondolewa timu ya waendesha baiskeli ya Israel kwenye mashindano ya mchezo huo, kufuatia maandamano na malalamiko ya waungaji mkono wa Palestina nchini humo.
……………………MWISHO………………