Ulimwengu wa Spoti, Sep 29
https://parstoday.ir/sw/news/event-i131386-ulimwengu_wa_spoti_sep_29
Natumai u mzima wa afya mpenzi msikilizaji popote pale ulipo. Karibu tuangazie baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbali mbali za dunia.
(last modified 2025-10-20T07:03:11+00:00 )
Sep 29, 2025 08:57 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Sep 29

Natumai u mzima wa afya mpenzi msikilizaji popote pale ulipo. Karibu tuangazie baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbali mbali za dunia.

Handiboli; Iran U17 bingwa wa Asia

Iran imeibuka kidedea katika Duru ya Kwanza ya Mashindano ya Mpira wa Mikono ya Wanaume wenye chini ya miaka 17 ya Asia. Iran ilishinda Korea Kusini kwa alama 28-25 katika mechi ya mwisho ya mashindano hayo Alkhamisi kwenye Ukumbi wa Bintimfalme Sumaya huko Amman, mji mkuu wa Jordan. Iran hapo awali iliishinda Korea Kusini 31-25 katika hatua ya awali. Mapema Alkhamisi, Qatar ilimaliza katika nafasi ya tatu kwa ushindi wa 33-26 dhidi ya Bahrain.

 

Iran ilizishinda Maldives, Syria, Korea Kusini (mara mbili), Kuwait, Jordan, Qatar, na Bahrian katika mashindano hayo kabla ya kutinga fainali. Mashindano hayo yametumika kama jukwaa la kufuzu kwa Mashindano ya Kwanza ya Dunia ya Mpira wa Mikono kwa Wanaume wenye chini ya miaka 17 ya IHF, yaliyoratibiwa kufanyika nchini Morocco kuanzia Oktoba 24 hadi Novemba Mosi. Iran na Korea Kusini, zitaliwakilisha bara la Asia kwenye Mashindano ya Dunia ya Handiboli.

Futsal Asia; Iran yaendelea kutoa dozi

Iran ambao ni mabingwa watetezi imeendelea vyema na kampeni yao ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Futsal la Asian zitakazopigwa Indonesia 2026, kwa ushindi mwingine wa mabao 10-0 dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu katika mchezo wa Kundi G uliopigwa Jumatatu. Iran, ambao waliichabanga Bangladesh mabao 12-0 katika mchezo wa ufunguzi Jumamosi ya wiki iliyopita, ilihitaji sekunde 30 pekee kupata bao kupitia kwa Behrooz Azimi.  Kuanzia hapo, mvua ya mabao iliendelea kushuhudiwa huku Imarati wakilambishwa sakafu.

Soka ya Vipofu: Iran yatamba

Iran iliichabanga Korea Kusini mabao 3-0 siku ya Jumapili, siku moja baada ya kuigaragaza India mabao 3-0 kwenye mchuano mwingine wa Kombe la Mataifa ya Vipofu la IBSA 2025 Jumamosi usiku. Morteza Karimi, Sadegh Rahimi na Mohammad Amin Rahimzadeh waliifungia Iran inayonolewa na kocha wa muda mrefu, Javad Felfeli. Mashindano haya ni hafla rasmi kwa nchi sita bora katika viwango vya IBSA vilivyotangazwa mnamo Januari 2025. Ni tukio rasmi la kwanza katika mzunguko mpya kuelekea Michezo ya Walemavu ijayo huko Los Angeles. Kufuatia kukamilika kwa mashindano ya wanaume, India itaandaa Mashindano ya Dunia ya Wanawake wasioona ya IBSA kati ya Oktoba 6 na 12.

 

Kabla ya hapo, Iran na Uingereza zilitoa sare tasa kwenye mchuano wa Kombe la Mataifa ya Wasioona la IBSA la 2025 Ijumaa. Iran, ambao walikuwa wameilaza Poland 4-0 katika mechi yao ya ufunguzi siku ya Alhamisi, wameratibiwa kucheza na India, Korea Kusini na Italia siku zinazofuata. Mashindano haya ni hafla rasmi kwa nchi sita bora katika viwango vya IBSA vilivyotangazwa mnamo Januari 2025. Ni tukio rasmi la kwanza katika mzunguko mpya kuelekea Michezo ya Walemavu ijayo huko Los Angeles.

Shirikisho la Soka Iran: Israel ipigwe kadi nyekundu

Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetoa wito wa kutimuliwa Israel katika soka kutokana na mauaji yake ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Msemaji wa Shirikisho la Soka la Iran amesema kuwa, wameliandikia Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mara kadhaa wakitaka kusimamishwa kwa Shirikisho la utawala wa kizayuni wa Israel. Amir Mehdi Alavi, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Umma wa Shirikisho la Kandanda la Iran amebainisha kuwa, Shirikisho la Soka la Iran limetuma barua mara kadhaa kwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na Shirikisho la Soka la Asia (AFC) likitaka kusimamishwa uanachama wa shirikisho la soka la utawala wa kizayuni wa Israel kutokana utawala huo ghasibu kutekeleza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

 

Wakati huo huo, Mkuu wa Shirikisho la Soka la Jordan ametangaza kuanza kwa mchakato rasmi na ulioratibiwa wa kusimamisha uanachama wa Shirikisho la Soka la Israel katika Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na Muungano wa Vyama vya Soka vya Ulaya (UEFA). Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Palestina zaidi ya wanamichezo 800 wameuawa shahidi tangu utawala haramu wa Israel ulipoanzisha hujuma na mashambulio ya kinyama dhidi ya Gaza Oktoba 2023.

Mashindano ya Olimpiki ya Asia

Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki ya Iran (NOC) imezindua kauli mbiu yake rasmi ya Michezo ya Vijana ya Asia ya 2025. Kauli mbiu ni "Tumaini la Iran" katika Michezo hiyo. Rais wa shirikisho la mpira wa mikono la Iran Alireza Pakdel ndiye mjumbe wa mpishi wa Michezo hiyo. Michezo ya tatu ya Vijana ya Asia itakuwa kwa mara ya kwanza Bahrain kuandaa mashindano ya Michezo ya Asia kwa kategoria ya vijana, kukaribisha washiriki kutoka nchi 45 ambao watashiriki katika michezo 24 na mashindano 253 katika maeneo mbalimbali nchini. Toleo la tatu la Michezo, tukio la michezo mingi la Pan-Asia litakalofanyika Bahrain kuanzia Oktoba 22 hadi 31, 2025. Litakuwa ni mara ya kwanza kwa toleo hilo kufanyika tangu lile la mwisho mwaka wa 2013.

Ligi ya Mabingwa Afrika

Klabu ya soka ya Simba ya Tanzania imesonga mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya Jumapili kutoka sare ya bao 1-1 na Gaborone United katika mchezo wa marudiano wa michuano hiyo. Katika mchezo huo wa marudiano dhidi ya Gaborone United, Jumapili, Septemba 29, 2025, Simba ilihitaji ushindi au sare ya aina yoyote ili iingie raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu. Katika mechi za kwanza ugenini, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 nchini Botswana na Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 huko Sudan Kusini.

Wekundu wa Msimbazi uwanjani

 

Kutokana na matokeo hayo Simba imefuzu kwa jumla ya mabao 2-1 kutokana na ushindi wa bao 1-0 iliyoupata mchezo wa kwanza baina ya timu hizo wiki iliyopita nchini Botswana. Kwa ushindi wa wikendi, Wekundu wa Msimbazi wameibuka na jumla ya magoli 2-1. Watani wa Simba, klabu ya Yanga wakiupigia nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, waliigaragaza Wiliete ya Angola mabao 2-0, na kusogea mbele kibabe. Mabao ya Wananchi katika mchezo huo wa nyumbani yalifungwa na Wafungaji ni Pacome Zouzoua na Aziz Andabwile. Yanga imesonga mbele kwa jumla ya magoli 5-0. Katika mechi za kwanza ugenini, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Wiliete huko Angola huku Singida Black Stars ikipata ushindi wa bao 1-0 huko Rwanda dhidi ya Rayon Sports na Mlandege ilifungwa mabao 2-0 na Ethiopian Insurance ya Ethiopia. Katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga itakutana na Silver Strikers ya Malawi.

Wachezaji wa Yanga wakilitandaza gozi

 

Huku hayo yakijiri, klabu nyingine ya soka ya Tanzania ya Azam FC imeng’ara kwa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya wikendi kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya El Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam. Azam FC sasa imesonga mbele kwa jumla ya mabao 4-0 baada ya mchezo wa kwanza kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 nchini Sudan.

Katika hatua nyingine, Maafande wa Kenya ambayo wiki iliyopita waliibamiza Mogadishu City ya Somalia mabao 3-1 katika mchuano wao wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa ya CAF katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, waliingiza mapuuza uwanjani na wajikuta wanalazimishwa sare ya mabao 3-3 katika matokeo jumla. Kenya Police walisonga mbele kwa sheria ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya jumla ya 3-3, na hivyo kuweka hai ndoto yao ya kihistoria ya kufika hatua ya makundi yenye faida kubwa. Maafande walianza mechi hiyo kwa kujiamini, wakifurahia kumiliki mpira lakini wakashindwa kugeuza ubabe wao kuwa nafasi za wazi.

Wakati huo huo, vijana 2 wa Kisomali wanaotuhumiwa kuivunjia heshima bendera ya Kenya wataendelea kuzuiliwa katika kitengo cha ulinzi wa watoto cha Gigiri hadi Oktoba 2. Wakili wa watoto hao, Ishamael Nyaribo amesema, "Watoto hao huenda walivuka mipaka katika kukanyaga bendera ya Kenya, na ingawa hilo halikubaliki, ni lazima warekebishwe ipasavyo kwa vile bado ni watoto." Waliinajisi bendera ya Kenya, ambayo ni moja ya nembo za taifa, wakati wa mchuano wao wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa ya CAF, ambapo Maafande wa Kenya Jumamosi ya wiki iliyopita, waliibamiza Mogadishu City ya Somalia mabao 3-1 katika mchezo uliopigwa uliopigwa katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi. Klabu ya Mogadishu City imetoa taarifa ya kuomba radhi kutokana na kitendo hicho kilichofanywa na mashabiki zake. Nairobi United imesogea mbele pia kwenye raundi ya pili, baada ya kutoa sare ya jumla ya mabao 3-3 na Uganda National Enterprise kwenye Kombe la Shirikisho la CAF.

Dondoo za Hapa na Pale

Timu ya polo ya wanaume ya Iran imenyimwa visa kwa ajili ya Mashindano ya Dunia ya FIP Arena Polo 2025, yatakayofanyika Marekani. Mashindano hayo yamepangwa kufanyika Crozet, Virginia, kuanzia Oktoba 5 hadi 12. Iran  ilijikatia tketi mwezi Mei katika mchujo uliofanyika Riyadh, Saudi Arabia.

Katika riadha, mwanaraiadha wa Kenya, Philemon Kiriago alishinda medali ya pekee ya dhahabu ya Kenya wakati Mashindano ya Dunia ya Mbio za Milima na Trail yaliyokamilika Jumapili huko Canfranc Pirineos, Uhispania. Kiriago ilimshinda Martin Kiprotich wa Uganda, huku Mkenya mwingine, Paul Machoka, akiibuka wa 3 katika mbio hizo za kilomita 14 za Mlima Classic za wanaume. Kenya ilinyakua medali za fedha na shaba katika siku ya ufunguzi wa mashindano hayo. Richard Atuya na Philemon Kipng’eno walishinda medali hizo mtawalia, katika mbio kilomita 6 za wanaume.

Ballon

 

Na tunamatisha na habari ya matumaini ambapo fowadi wa klabu ya PSG na Ufaransa, Ousmane Dembele alishinda tuzo ya Ballon d'Or kwa upande wa wanaume kwenye hafla iliyofanyika kwneye ukumbi wa Theatre du Chatelet mjini Paris Jumatatu iliyopita Septemba 22. Alimbwaga mshambuliaji wa Uhispania na Barcelona Lamine Yamal, huku mwenzake wa PSG Vitinha akishika nafasi ya tatu.

…………………MWISHO………………