Aug 06, 2023 07:22 UTC

Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Iran amesema usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman na Bahari Hindi hauna mfungamano wowote na Marekani.

Abolfazl Shekarchi, Msemaji wa Jeshi la Iran alisema hayo jana Jumamosi, akijibu mpango wa Marekani wa kutaka kutuma askari wake kusindikiza meli za kibiashara zinazopita Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz. 

Amesema nchi za eneo la Asia Magharibi zina uwezo wa kudhamini usalama wa maji ya kanda hii, pasi na kuhitaji msaada wa Marekani.

Shekarchi ameihubutu Washington kwa kuhoji kuwa: Usalama wa Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman na Bahari Hindi una mfungamano gani na Marekani? Vikosi vya Marekani vinafanya nini katika eneo?"

Kamanda huyo mwandamizi wa Jeshi la Iran amesisitiza kuwa, usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman na Bahari Hindi hauna mfungamano wowote na Marekani, na kwamba nchi za eneo la Asia Magharibi zina uwezo wa kujidhaminia usalama wao.

Brig. Jen. Abolfazl Shekarchi, Msemaji wa Jeshi la Iran

Kauli ya Msemaji wa Jeshi la Iran imekuja siku chache baada ya Marekani kusema kuwa itatuma askari, ndege za kivita na manowari za kijeshi kutoa ulinzi kwa meli za kibiashara zinazopita katika maji ya Ghuba ya Uajemi, ikiwa ni hatua nyingine ya kichokozi na uingiliaji wa kijeshi katika eneo hili la kistrateji.

Shekarchi ameongeza kuwa, ni katika sera za Marekani kuilaumu nchi ya tatu kwa ukosefu wa usalama katika eneo la Asia Magharibi, na kutumia suala hilo kuimarisha uwepo wake wa kijeshi katika maji ya eneo hili. 

Tags