Aug 07, 2023 12:48 UTC
  • Iran: Chokochoko za NATO ni miongoni mwa sababu kuu za vita vya Ukraine

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amir-Abdollahian amegusia juhudi za Tehran kuelekea suluhisho la kisiasa la mgogoro wa Ukraine na kusisitiza kuwa muungano wa kijeshi wa NATO unaoongozwa na Marekani na chokochoko ulizofanya ni miongoni mwa sababu zilizopelekea kuzuka mgogoro huo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Japan, Tokyo, Amir-Abdollahian amesema: "tunaichukulia NATO na uchochezi wake kuwa ni kati ya sababu kuu za vita na mgogoro uliopo. Tunaendeleza juhudi zetu za kusitisha vita na kuzifanya pande zingine zizingatie suluhisho la kisiasa".

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza pia kuwa Jamhuri ya Kiislamu siku zote imeshikamana na misimamo yake yenye misingi mikuu inayosisitiza kuwa vita si suluhisho la mgogoro.

Waziri Hossein Amir-Abdollahian katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Tokyo

Amefafanua kuwa, tangu vilipoanza vita, Iran imekuwa ikifuatilia ajenda ya kukomesha vita hivyo na kuzihimiza pande husika zirudi kwenye meza ya mazungumzo na kutafuta suluhisho la kisiasa, sambamba na kuchukua hatua za dhati kupitia utaratibu huo.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekanusha kwa mara nyingine tena na kusisitiza kuwa "ni makosa na si sahihi hata kidogo" shutuma zinazotolewa za kutumika ndege zisizo na rubani za Iran katika vita vya Ukraine.

Amesema, ushirikiano wa kiulinzi wa Iran na Russia haujawahi kuhusisha matumizi ya ndege zisizo na rubani au silaha za Iran katika vita vya Ukraine kwani Russia yenyewe ni mojawapo ya waundaji na wauzaji wakubwa wa silaha duniani.../

Tags