Rais Ibrahim Raisi: Iran iko tayari kushirikiana na Tanzania katika nyuga mbalimbali
(last modified Fri, 25 Aug 2023 03:10:09 GMT )
Aug 25, 2023 03:10 UTC
  • Rais Ibrahim Raisi: Iran iko tayari kushirikiana na Tanzania katika nyuga mbalimbali

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza utayarifu wa Iran wa kushirikiana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nyanja mbalimbali kama za kutoa huduma za uhandisi wa kiufundi, ujenzi wa mabwawa, mitambo ya kuzalisha umeme, kilimo na viwanda.

Rais Ibrahim Raisi amesema hayo pambizoni mwa mkutano wa Kundi la Brics mjini Johannesburg Afrika Kusini katika mazungumzo yake na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusisitiza kwamba, Iran ina azma ya kukuza zaidi ushirikiano wake na Tanzania.

Rais wa Iran amekaribisha kwa mikono miwili kupanuliwa ushirikiano wa pande mbili na kusisitiza juu ya kuanzishwa kwa tume ya pamoja ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili, pamoja na kupanga mipango ya kuboresha kiwango cha mahusiano ya kiuchumi na kiutamaduni.

 

Kwa upande wake, Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sambamba na kukaribisha uanzishaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Iran, amesema: Iran na Tanzania zina uhusiano wa kirafiki wa kisiasa na kidiplomasia, na uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili unapaswa kukua kwa mujibu wa mahusiano haya.

Aidha pambizoni mwa mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Kiiislamu ya Iran amekutana na viongozi mbalimbali wakiwemo Marais wa China, Senegal na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na viongozi wengine ambapo amebadilisha mawazo kuhusiana na masuala mbalimbalii kama uhusiano wa pande mbili na matukio ya kieneo na kimataifa.