Sep 23, 2023 04:08 UTC
  • Iran na Djibouti zakubaliana kufufua uhusiano wa kidiplomasia

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Djibouti wameafikiana juu ya kuhuisha uhusiano wa kidiplomasia wa Tehran na Asmara, kwa maslahi ya mataifa haya mawili.

Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mwafaka huo umepatikana katika mazungumzo yake na mwenzake wa Djibouti, Mahamoud Ali Youssouf, pambizoni mwa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.

Amir Abdollahian amesema katika mazungumzo hayo kwamba, Iran na Djibouti zilikuwa na uhusiano mzuri katika miaka ya huko nyuma, na kwa msingi huo mataifa haya yana historia ya ushirikiano wa pande mbili katika nyuga mbalimbali.

Amesema, "Tunaitazama Djibouti kama nchi rafiki na ya kidugu. Iran inalichukulia kwa uzito suala la kupanua mahusiano yake na Djibouti kama nchi muhimu ya Waislamu katika eneo la Pembe ya Afrika."

"Tunaweza kuimarisha uhusiano wetu pamoja na kupanua ushirikiano wa pande mbili katika nyuga tofauti," ameongeza Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran. Wanadiplomasia hao wa ngazi za juu wa Iran na Djibouti wamesisitizia haja ya kupigwa jeki ushirikiano wa mataifa haya mawili katika nyuga tofauti kama vile uwezekaji, biashara, ubunifu wa sayansi na teknolojia

Itakumbukwa pia kuwa, tarehe 6 Januari mwaka 2016, serikali ya Djibouti ilitangaza kuwa, nchi hiyo ndogo ya Pembe ya Afrika imeamua kukata uhusiano wake na Iran ili kufuata siasa za Saudi Arabia. 

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Misri mjini New York

Wakati huohuo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Misri, Sameh Shoukry mjini New York, ambapo wamezungumzia juu ya kufufuliwa uhusiano kamili wa kidiplomasia wa nchi mbili hizi.

Shoukry amesema Misri ina hamu ya kuwa na uhusiano chanya na Iran huku akisisitiza kwamba, hakuna wakati wowote mawasiliano baina ya nchi mbili hizi umekatika.

Tags