IRGC:Uchu wa kuikomboa Quds, chachu ya harakati za muqawama
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran IRGC limesema uchu wa kutaka kukombolewa Quds tukufu ndio chachu inayozipa nguvu harakati za kimuqawama katika eneo hili la Mashariki ya Kati.
Taarifa ya IRGC kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds imesema kuwa, harakati za muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni zinazidi kupata nguvu na kuimarika siku baada ya siku kutokana na raghba ya wanamuqawama kutaka kuikomboa Quds tukufu sanjari na kuwakomboa wananchi madhulumu wa Palestina kutoka kwa minyororo ya ubeberu na jinai za utawala haramu wa Israel. Taarifa hiyo ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu imeongeza kuwa, utawala ghasibu wa Israel ndio adui nambari moja unaostafidi na ukosefu wa usalama na uthabiti katika eneo hili na kusisitiza kwamba, Intifadha ya 3 ya kuikomboa Quds tukufu imefanya kila kona ya ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu kutokuwa salama kwa walowezi wa Kizayuni. Kadhalika taarifa hiyo imewataka wananchi wa Iran kushiriki kwa wingi katika maandamano ya leo kote nchini. Hii ni katika hali ambayo, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran naye pia amelitaka taifa la Iran na Waislamu kote duniani kushiriki kwa wingi katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds hii leo.