Oct 19, 2023 06:06 UTC
  • Iran na Tunisia zafanya mazungumzo ya namna ya kuwasaidia wananchi wa Ghaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Tunisia mjini Jeddah, Saudi Arabia na pande mbili zimejadiliana njia za kuwasaidia wananchi wa Ghaza na kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni.

Pande mbili za Iran na Tunisia zimejadiliana pia njia za kukabiliana na hatua zinazotokana na misimamo mikali ya Kizayuni dhidi ya taifa la Palestina na kutumia machaguo mengine hasa muqawama katika kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, mkutano huo ulifanyika jana Jumatano pambizoni mwa kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kilichoitishwa mjini Jeddah kwa ajili ya kuzungumzia jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza.

Mawaziri hao wawili, Hossein Amir-Abdollahian wa Iran na Nabil Ammar wa Tunisia wote wawili wametilia mkazo msimamo usiotetereka wa nchi zao katika kuliunga mkono taifa la Palestina.

Nchi mbili ndugu za Iran na Tunisia zina mambo mengi ya kuimarisha uhusiano wao kwenye nyuga zote

 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, vitendo vya kuchupa mipaka vya utawala wa Kizayuni dhidi ya taifa la Palestina havina chaguo jingine isipokuwa kuendesha muqawama wa pande zote dhidi ya utawala huo dhalimu.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia ameelezea kufurahishwa kwake na fursa ya kuzungumza na Waziri mwezake wa Mambo ya Nje wa Iran na kusema: Sisi tunaamini kwamba kuiunga mkono kadhia ya Palestina ni kuunga mkono kadhia ya haki.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Tunisia amegusia pia uhusiano wa jadi baina ya nchi yake na Iran na kusema kuwa, kuna wajibu wa kutumiwa uwezo na fursa zote zilizopo kuhakikisha kwamba uhusiano wa nchi hizi ndugu unaimarika zaidi katika nyuga zote.

Tags