Abdollahian aiambia US: Acheni mauaji ya kimbari, undumakuwili Gaza
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekosoa undumakuwili wa Marekani ambayo kwa upande mmoja inadai kuwa inataka usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza, na kwa upande mwingine inaendelea kuunga mkono utawala wa Kizayuni ambao unaendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo lililo chini ya mzingiro.
Hossein Amir-Abdollahian ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kuwa, Wamarekani wameitumia Iran ujumbe wakidai kuwa wanataka usitishaji vita Gaza, katika hali ambayo wameendelea kuuunga mkono utawala wa KIzayuni katika mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya wakazi wa Gaza.
Amesema: Marekani imekuwa ikitaka usitishaji vita wa kibinadamu tangu wiki iliyopita. Tunatumai karibuni hivi Washington itabadili sera zake na iache kuunga mkono utawala ghasibu.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameihutubu Marekani katika ujumbe wake huo kwa kusema: Acheni undumakuwili na mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza.
Abdollahian ameongeza kuwa, kuharibiwa na kubomolewa kwa makusudi miundombinu ya mji na idara, hospitali, vituo vya elimu na shule kuwa ni jambo la kutisha kwa ulimwengu kuwahi kulishuhudiwa katika karne ya karibuni.
Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza kuwa, watu zaidi ya 10,000 wameuliwa shahidi katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7 hadi sasa; ambapo kati ya mashahidi hao watoto ni 4,800, wanawake 2,550 na wazee 596.
Wizara hiyo aidha imetangaza kuwa watu elfu 24 na 808 wamejeruhiwa hadi sasa katika mashambulizi ya kikatili ya utawala haramu wa Israel huko Gaza.