Iran: Afrika ina hamu ya kufufua utambulisho wake
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Anayehusika na Masuala ya Kisiasa amesisitizia haja ya kuimarishwa uhusiano na ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu na nchi za Afrika ikiwemo Senegal katika nyuga mbalimbali.
Ali Baqeri Kani ametoa mwito huo katika mazungumzo yake na Spika wa Bunge la Senegal, Amadou Mame Diop mjini Dakar na kuongeza kuwa, kufanyika mara kwa mara mkutano wa Baraza la Amani na Usalama (PSC) kunaashiria hamu ya Senegal ya kuhuisha utambulisho wa Afrika na kuimarisha uhuru wa mataifa ya bara hilo.
Amesema Iran na Senegal zina historia ya jadi, na mataifa haya mawili yana uwezo wa kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika nyuga tofauti kama vile siasa, uchumi na hata ushirikiano wa mabunge ya nchi hizi.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Senegal, Amadou Mame Diop mbali na kuishukuru Iran kwa kushiriki kwenye mkutano wa Baraza la Amani na Usalama (PSC) mjini Dakar, amesisitiza kuwa mataifa haya mawili yana fursa ya kupanua zaidi mahusiano yao katika nyuga mbalimbali.
Amesema nchi yake ina hamu ya kuimarisha ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga za kilimo, nishati, viwanda na madini.
Aidha Spika wa Bunge la Kitaifa la Senegal amesema sera na msimamo wa nchi hiyo ya kuliunga mkono taifa la Palestina ipo imara.
Ikumbukwe kuwa, Februari mwaka huu, ujumbe wa ngazi ya juu wa kiuchumi wa Senegal ukiongozwa na mshauri mkuu wa rais na mkuu wa chama cha wafanyakazi cha nchi hiyo uliitembelea Iran kwa ajili ya kuimairisha ushirikiano wa kiuchumi wa pande mbili.
Biashara kati ya Iran na Senegal mwaka uliopita ilifikia thamani ya dola milioni 2 na laki nne, ambapo asilimia 50 ni sehemu ya mauzo ya vipuri vya magari na pikipiki, na asilimia 17 ya hiyo ni sehemu ya mauzo ya bidhaa za chakula nje ya nchi. Vilevile kiasi cha uagizaji bidhaa kutoka Senegal kuja Iran katika muda huo kilikuwa cha karibu dola laki 3.7.