Dec 04, 2023 02:59 UTC
  • Safari ya Rais wa Cuba mjini Tehran

Rais wa Jamhuri ya Cuba ambaye anangoza ujumbe wa ngazi ya juu wa kisiasa na kiuchumi wa nchi yake amefanya safari mjini Tehran kwa mwaliko rasmi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rais Miguel Díaz-Canel wa Cuba, amefanya safari nchini Iran miaka 22 baada ya ziara ya mwisho ya hayati Rais Fidel Castro mjini Tehran, amekutana na Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na viongozi wengine wakuu nchini. Canel na ujumbe anaoandamana nao pia watatembelea maonyesho ya uwezo na mafanikio ya kiteknolojia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Safari hii inafanyika huku Iran na Cuba hususan katika miaka ya hivi karibuni zikiwa zimetilia mkazo suala la kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi, ambapo viongozi wa nchi hizi mbili wamefanya safari mbalimbali mjini Tehran na Havana ili kupanua ushirikiano wa pande mbili.

Zikiwa ni nchi zilizo mbali kijiografia, Iran na Cuba zimekuwa zikifuatilia malengo ya pamoja ambayo yamezipelekea kuwa karibu zaidi kisiasa na kiuchumi. Kujitengemea na kutofungamana na siasa za madola ya kibeberu, kupinga ubeberu, kutengemea uwezo wa  ndani, kuunga mkono harakati za ukombozi na kuunga mkono wanyonge duniani ni miongoni mwa itikadi za pamoja kati ya Iran na Cuba, ambapo nchi zote mbili zimeshuhudia mapinduzi ya wananchi.

Rais Miguel Díaz-Canel wa Cuba

Wakati huo huo, mapambano dhidi ya uingiliaji wa Marekani yanachukuliwa kuwa jambo la kawaida kabisa kati ya Tehran na Havana. Tangu mwanzoni mwa miaka ya 1960, Marekani iliiwekea vikwazo Cuba kutokana na sera zake za kimapinduzi na kutoitegemea Washington, vikwazo ambavyo vimekuwa vikitekelezwa kwa makali zaidi dhidi ya Tehran tangu mwanzoni mwa miaka ya 1980 kufuatia Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Nchi mbili hizi ambazo zimestahamili mashinikizo makali ya kiuchumi kutokana na vikwazo vya Marekani, zimeweza kudhihiri kama mfano uliofanikiwa pakubwa katika kuzima na kupunguza makali ya vikwazo vya Marekani. Licha ya kutokuwa na maliasili nyingi, Cuba imeweza kupata mafanikio makubwa katika nyanja za afya, matibabu na elimu, kiasi cha kufikia hatua ambayo baadhi ya nchi za eneo la Amerika ya Latini zinaomba kunufaika na bidhaa na huduma za afya, ufundi na sayansi kutoka Cuba.

Katika miongo ya hivi karibuni, Iran imeweza kushinda vikwazo vya Marekani, na kukidhi mahitaji yake ya msingi pamoja na kupiga hatua kubwa za ustawi na maendeleo katika nyanja tofauti za sayansi na viwanda kama vile vyombo vya anga na ulinzi.

Uzoefu huu wa pamoja kati ya Iran na Cuba umepelekea nchi mbili hizi kushirikiana ili kukidhi mahitaji yao na vilevile kuzinufaisha nchi nyingine.

Katika safari hii ya Rais wa Cuba nchini Iran, uhusiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya nchi mbili unatazamiwa kuimarishwa pakubwa kwa kuzingatia uwiano wa kisiasa na kiuchumi.

Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuhusiana na hilo: Iran na Cuba ni waanzilishi wa mafungamano ya kieneo, jambo ambalo linaweza kutoa fursa ya uwepo wao katika miungano mpya inayodhihiri katika pande mbili za dunia, na mazingatio makubwa bila shaka yatakuwa katika nyanja za bioteknolojia, ufundi, matibabu na nishati.

Kwa upande mwingine, kutetea taifa madhulumu la Palestina ni sifa ya pamoja ya mataifa mawili ya Iran na Cuba. Nchi hizi zinaunga mkono kwa dhati kadhia ya taifa la Palestina na mara zote zimekuwa zikilaani jinai za Israel dhidi ya raia wa Palestina katika majukwaa tofauti ya kimataifa. Huku jinai mpya zikiwa zinatekelezwa na Wazayuni dhidi ya watu wa Gaza ambapo mauaji ya kizazi ya kutisha yanatekelezwa dhidi ya taifa la Palestina, viongozi wa Tehran na Havana wameimarisha misimamo yao ya kuwatetea Wapalestina.

Cuba daima imekuwa mtetezi wa haki za Wapalestina

Norma Guicochea, Mkuu wa Jumuiya ya Cuba katika Umoja wa Mataifa, hivi karibuni na kwa niaba ya mashirika ya kiraia ya nchi hiyo alisisitiza uungaji mkono wake kwa malengo ya kiadilifu ya taifa la Palestina kwa kusema: "Ukaliaji mabavu wa ardhi na kulazimishwa familia za Wapalestina kuyahama makazi yao, ni aibu kwa jamii ya wanadamu."

Msimamo huo unaowiana na misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu Palestina unaweza kuongeza mashinikizo dhidi ya utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake wa nchi za Magharibi.

Tags