Feb 04, 2024 02:53 UTC
  • Rais wa Iran: Tumesambaratisha vikwazo

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Kurushwa kwa satalaiti 11 za Iran kwa mafanikio kumeshinda vikwazo vya Marekani na Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Seyed Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumamosi amehutubia sherehe za Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Anga za Mbali na kusisitiza kuwa, nchi kuweza kufika katika anga za mbali ni chanzo cha nguvu, matumaini na utajiri. Ameendelea kusema kuwa maadui walijaribu kusimamisha mchakato wa ustawi wa Iran na kuitenga nchi hii lakini kurushwa kwa satelaiti 11 katika anga za mbali kwa mafanikio kumesambaratisha vikwazo na njama zote za kuitenga Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema licha ya vitisho na vikwazo vyote hivyo, Iran imedhihirisha kuwa inaweza  kugeuza vitisho na vikwazo hivyo kuwa fursa ya ustawi na kwa msingi huo ndio imeweza kurusha satalaiti kadhaa katika anga za mbali.

Amesema mafanikio hayo yenye thamani yamefikiwa   kwa ushirikiano wa vijana na hasa wasomi, na majeshi ya Iran, na ushirikiano huo umeweza kuiletea nchi heshima na fahari.
Raisi ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kati ya nchi 10 bora duniani katika uga wa anga za  mbali.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliashiria pia maadhimisho ya siku zenye baraka za Alfajiri 10 ambazo ni kielelezo cha maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kubainisha kuwa taifa ambalo liliamua kupata uhuru kamili na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu na maendeleo ya nchi mnamo 22 Bahman (Februari 11, 1979) sasa linataka kupata ushindi mwingine.

Tags