Feb 09, 2024 07:40 UTC
  • Nasser Kan'ani
    Nasser Kan'ani

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa hatua ya jeshi la magaidi la Marekani ya kumuuwa shahidi mmoja wa viongozi wa harakati ya wapiganaji wa kujitolea ya Iraq ni katika mlolongo wa kudumisha himaya na uungaji mkono kamili wa serikali ya Marekani kwa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Palestina.

Taarifa hiyo imetolewa baada ya vikosi vya jeshi la kigaidi la Marekani vilivyoko katika eneo la Asia Magharibi, Asia ya Kati na Afrika Mashariki (Centcom) kumuua Abu Baqir al-Saa'di, mmoja kati ya viongozi wa harakati ya wapiganaji wa kujitolea ya wananchi wa Iraq maarufu kama al Hashd al-Shaabi) Jumatano iliyopita, kwa kutumia ndege isiyo na rubani ambayo ilishambuliwa gari lake mjini Baghdad, Iraq.

Shambulio hilo la kigaidi limefuatiwa na malalamiko makali ya maafisa wa serikali ya Iraq na vyama vya siasa; Huku Wairaqi wakilaani kitendo hicho na kutoa wito wa kukomeshwa uwepo wa majeshi ya Marekani nchini humo.

Shirika la Habari la Iran, IRNA limeripoti kuwa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan'ani amelaani vikali kitendo cha kigaidi cha serikali ya Marekani nchini Iraq, ambacho kilipelekea kuuawa shahidi wanachama kadhaa wa harakati za kujitolea za kupambana na ugaidi za wanchi, akiwemo Abu Baqir Al-Saa'di aliyeongoza mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh. Kan'ani amesema shambulizi hilo la Marekani ni mfano wa wazi wa ugaidi wa kiserikali na "ukiukwaji wa uhuru wa kujitawala" na kwamba limekiuka sheria na kanuni za kimataifa.

Amesema: Kuendelea kwa vitendo kama hivi vya Marekani ni tishio kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kwa mara nyingine tena amesisitiza wajibu wa jamii ya kimataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kukomesha vitendo na mashambulizi yanayokiuka sheria ya Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia na kuzuia kupanuka zaidi mizozo na ukosefu wa amani.

Tags