Mar 13, 2024 07:46 UTC
  • Iran na Iraq zasisitizia haja ya kusimamishwa mauaji ya kimbari Gaza

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Iraq wametoa mwito wa kuchukua hatua zaidi hasa za kisiasa kwa ajili ya kusimamisha mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Katika mazungumzo yao ya simu jana Jumanne, Hossein Amir-Abdollahian na Fuad Hussein, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Iraq wamejadili matukio ya Gaza na kuitaka jamii ya kimataifa kuwatumia Wapalestina wa ukanda huo uliozongirwa misaada ya kibinadamu haraka iwezekanavyo. 

Wanadiplomasia hao wa Iran na Iraq wamezitaka nchi za Kiislamu kuchukua hatua madhubuti za kukomesha mauaji ya halaiki na uhalifu wa kivita wa utawala wa kibaguzi wa Israel huko Gaza.

Viongozi hao wamesisitiza kwamba, suala la Palestina ni kadhia kuu ya Umma wa Kiislamu, na hivyo wametoa mwito kwa mataifa ya Kiislamu kuchukua hatua za kuwanusuru wenzao wa Palestina. 

Aidha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Iraq wameashiria uhusiano wa nchi mbili hizi na kusisitiza kuwa, ushirikiano wa Tehran na Baghdad ni wa kuridhisha lakini kuna fursa za kuuimarisha zaidi.

Aidha viongozi hao wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq wametoa mwito wa kutekelezwa makubaliano ya pande mbili yaliyosainiwa na viongozi wa nchi mbili hizi jirani.

Kadhalika wameashiria umuhimu wa suala la usalama kwa Iran na Iraq na kubainisha kuwa, kukabiliana na makundi ya kigaidi na yanayotaka kujitenga katika maeneo ya mipakani kunahitaji ushirikiano na mchango wa nchi zote mbili.

 

Tags