Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aonana na watungaji tungo za kishairi
Jioni ya jana Jumatatu ambayo ilisadifiana na usiku wa mwezi 15 Ramadhani, siku ya kukumbuka alipozaliwa Imam Hassan al Mujtaba AS, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alionana na jamii ya washairi na watu wa sanaa na utamaduni na kuzungumza nao kwa karibu na kwa mapenzi makubwa.
Mazungumzo hayo yalifanyika kabla ya adhana ya Magharibi ambapo kwanza wasanii na washairi hao walionana na Kiongozi huyo Mkuu wa kidini wa Iran na baadaye Kiongozi Muadhamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aliwasalisha hadhirina Sala za Maghrib na Isha sambamba na kula nao futari.
Kiongozi Muadhamu amesema, tungo za kishairi zenyewe ni chombo madhubuti cha kuwatangazia walimwengu changamoto mbalimbali, vita na matukio chungu nzima yanayotokea duniani.
Amesema athari za vyombo vya mawasiliano ya umma ni kubwa zaidi kuliko hata makombora, droni na ndege za kivita na kwamba kila mwenye chombo kikubwa na chenye nguvu zaidi cha habari hufanikiwa kufikia malengo yake.
Katika sehemu nyingine ya miongozo yake kwenye mjumuiko huo, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametilia mkazo udharura wa kuweko mwamko na mapinduzi ya kufasiriwa kwa lugha nyingine athari zenye thamani kubwa za wasanii wa Iran akitoa mfano kwa kusema kuwa, kwa mfano lau kama tungo za washairi hao kuhusu Ghaza zingefasiriwa kwa lugha nyingine zingeweza kutoa athari kubwa na kuamsha hisia za walimwengu kuhusu mapambano ya wananchi wanamuqawama wa Palestina.
Aidha amesema, tungo za lugha ya Kifarsi lazima ziwe zinafikisha mafundisho na ujumbe wa kidini na kiustaarabu ikiwa ni pamoja na kuakisi muqawama na kusimama kidete na kishujaa taifa la Iran mbele ya mazingira tofauti magumu.