Rouhani: Iran itaendelea kupambana na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i11056-rouhani_iran_itaendelea_kupambana_na_ugaidi
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Iran itaendelea kutetea heshima na hadhi ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) kupitia njia ya kupambana na ugaidi bega kwa bega na wananchi na serikali ya Iraq.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 11, 2016 12:30 UTC
  • Rouhani: Iran itaendelea kupambana na ugaidi

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Iran itaendelea kutetea heshima na hadhi ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) kupitia njia ya kupambana na ugaidi bega kwa bega na wananchi na serikali ya Iraq.

Rais Rouhani ameyasema hayo leo mjini Tehran katika mazungumzo yake na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq, Sayyid Ammar Hakiim. Ameongeza kuwa ushindi wa hivi karibuni wa serikali na taifa la Iraq dhidi ya magaidi ni mafanikio yenye umuhimu mkubwa. Vilevile amesisitiza udharura wa kulindwa na kuimarishwa umoja na mshikamano wa ndani kati ya makundi yote ya kisiasa, kimadhehebu na kikabila nchini Iraq.

Rais Rouhani pia amepongeza nafasi ya viongozi wakuu wa kidini katika kuwaongoza wananchi na kuimarisha umoja na mshikamano kati ya makundi mbalimbali na akasema ustawi wa uhusiano wa Iran na Iraq utawanufaisha wananchi wa nchi hizo mbili na mataifa ya Mashariki ya Kati.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq amesema kuwa ushindi mkubwa wa kukombolewa Falluja kutoka kwenye makucha ya magaidi wa Daesh ni matokeo ya umoja na mshikamano wa makundi yote ya kisiasa, wananchi na jeshi la Iraq na amesisitiza umuhimu wa kudumishwa mshikamano huo hadi magaidi wa kitakfiri watakpofutwa kikamilifu.