Apr 20, 2024 02:59 UTC
  • Iran na Uturuki zatilia mkazo wajibu wa kukomeshwa haraka mashambulizi huko Ghaza

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki wamehimiza na kutilia mkazo udharura wa kukomeshwa mara moja mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye Ukanda wa Ghaza.

Hayo yameripotiwa na shirika la habari la IRNA ambalo limesema kuwa, Hossein Amir Abdollahian na Hakan Fidan, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Uturuki wamefanya mazungumzo kwa njia ya simu na kujadiliana matukio mbalimbali ya eneo hili vikiwemo vita vya Ghaza na wote wamezungumzia wajibu wa utawala wa Kizayuni kukomesha mara moja jinai zake za kuua kwa umati watoto, wanawake na raia wa kawaida huko Ghaza.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amegusia matamshi ya kichochezi ya viongozi wa utawala wa Kizayuni katika eneo la Asia Magharibi na kutilia mkazo umuhimu wa kufanyika juhudi za pande zote na za watu wote kuhakikisha Israel inakomesha mashambulizi yake huko Ghaza na hivyo kuuepusha ukanda huu na mgogoro wa kieneo na kimataifa. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, hadi hivi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel umeshaua kikatili na kwa umati zaidi ya Wapalestina 34,000 tangu tarehe 7 Oktoba 2023 wakati ilipouvamia ukanda huo wa Ghaza ambao umezingirwa kila upande na Israel kwa miaka mingi sasa.

Tags