Apr 22, 2024 13:20 UTC
  • Juhudi kubwa za Iran za kupunguza umaskini na kuongeza ustawi katika jamii

Takwimu mpya zilizochapishwa na Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa, umaskini mutlaki umepungua kwa kiasi kikubwa nchini Iran katika miaka ya hivi karibuni.

Shirika hilo la kimataifa limearifisha umaskini mutlaki kulingana na mapato ya kila siku ya dola 2.15 kwa kila mtu, na hiki ni kiasi cha chini ambacho mtu anahitaji ili kukidhi mahitaji yake ya msingi. Umaskini mutlaki una maana ya mtu mwenye kipato cha chini ya dola moja kwa siku. 

Kwa msingi huo, mnamo 2020, uwiano wa idadi ya watu maskini mutlaki ikilinganishwa na idadi ya watu nchini Irani ulikuwa 0.8%, lakini takwimu hii ilipungua hadi 0.7% mnamo 2021 na hadi 0.5% mwaka 2022.

Kwa utaratibu huo, umaskini mutlaki nchini Iran umepungua kwa 37% kwa miaka miwili mfululizo ikilinganishwa na mwaka 2020. Asilimia 0.5 ya kiwango cha umaskini mutlaki nchini Iran ndicho kiwango cha chini zaidi kilichorekodiwa katika miaka 5 iliyopita.

Katika miongo ya karibuni, kutokomeza umaskini uliokithiri nchini daima kumetangazwa kuwa mojawapo ya programu kuu za serikali. Ingawa, kwa mujibu wa viashiria vya kimataifa, hali ya Iran katika suala la umaskini ni bora zaidi ikilinganishwa na baadhi ya nchi za eneo la Magharibi mwa Asia, lakini kwa sababu mbalimbali, suala la kupambana na umaskini linahitaji mpango mpana na wa pande zote. Katika Serikali ya Awamu ya 13 ya Iran, suala la kufanyika mageuzi limepewa kipaumbele cha kwanza ikiwa ni pamoja na mageuzi katika muundo wa bajeti ya serikali, mageuzi katika muundo wa biashara na usafirishaji, mageuzi katika nyanja ya uzalishaji, uwekezaji na ajira, na hatimaye suala la kupunguza umaskini na kusaidia makundi yaliyo katika mazingira magumu.

Kuondoa utegemezi wa bidhaa za msingi na za kila siku za watu kwa fedha za kigeni, kupunguza pengo baina ya matabaka ya watu katika jamii kwa kubadilisha na kurekebisha sera za uchumi, kuweka uwiano baina ya mishahara na mfumuko wa bei, kusaidia familia na vikundi vyenye uwezo mdogo na kadhalika ni miongoni mwa ahadi zilizotolewa na Serikali ili koboresha maisha ya jamii, jambo ambalo kwa bahati nzuri limeambatana na hatua za kivitendo.

Miongoni mwa hatua zilizofanikiwa katika uwanja wa kupunguza umaskini na kuongeza ustawi wa umma katika miaka miwili iliyopita ni pamoja na kuzidhaminia chakula na ruzuku familia zenye kipato cha chini na kusaidia kupunguza mfumuko wa bei, kuongeza pensheni kwa wastaafu na utoaji wa nyumba makazi kwa walemavu. 

Pamoja na hayo yote, wataalamu wanasema, sera kuu inayopaswa kutekelezwa na Serikali ili kuboresha hali ya uchumi na ustawi wa watu ni kuthabitisha bei ya bidhaa mbalimbali na kuepuka kupanda bei hizo sambamba na kupambana na mfumuko wa bei katika hatua zote za kiuchumi. Hii ni kwa sababu, sera zinazosababisha mfumuko wa bei ndio chanzo kikuu cha umaskini katika jamii.

Kwa upande mwingine, sisitizo la serikali la kuegemea kwenye nguvu kazi na uzalishaji zaidi wa ndani, kubadilisha mwelekeo katika uhusiano na nchi za dunia kupitia makubaliano makubwa kama vile Mkataba wa Shanghai, BRICS, kutayarishwa fursa na uhusiano mpya na nchi jirani na kadhalika, yote hayo yanaonyesha jinsi Serikali ya Awamu ya 13 ilivyoazimia kutumia vyema nguvu kazi ya ndani na uwezo na fursa za kimataifa ili kuboresha hali ya maisha ya watu wa jamii ya Iran.