Apr 25, 2024 11:17 UTC
  • Ushauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi kuhusu kutumia vikwazo kama fursa ya maendeleo

Akiashiria nafasi muhimu ya jumuiya ya wafanyakazi katika kuongeza uzalishaji na kuboresha hali ya kiuchumi ya Iran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu katika sekta mbalimbali hususan silaha kuwa ni mfano wa kugeuza vikwazo kuwa fursa.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikikabiliwa na vikwazo vya Marekani na nchi nyingine za Magharibi.

Moja ya malengo muhimu ya Marekani katika kuendelea kuzidisha vikwazo ni kujaribu kuipigisha magoti Iran, kwa sababu Jamhuri ya Kiislamu imechukua sera huru zinazokinzana na Marekani, na hadi sasa mashinikizo ya pande zote ya Marekani na waungaji mkono wake hayajaweza kuvuruga utekelezaji wa sera huru za Iran.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu siku ya Jumatano katika kikao na kundi la wafanyakazi alibainisha uundwaji wa fursa kutokana na uadui wa maadui kuwa ni sifa ya kila taifa lililo hai na kuongeza kuwa, lengo la Marekani na Magharibi katika kulazimisha vikwazo na mashinikizo dhidi ya Iran limekuwa ni kutaka kulilazimisha taifa na mfumo wa utawala wa Kiislamu hapa nchini kusalimu amri na kutii kikamiilifu matakwa yao.  Amesisitiza kuwa: 'Taifa kubwa la Kiislamu na lenye historia ndefu halitasalimu amri mbele ya uonevu na sera za kutumia mabavu, na litapata mustakbali mzuri kwa kugeuza vikwazo kuwa fursa za maendeleo na ustawi.'

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamukatika kikao na kundi la wafanyakazi

Amesema ustawi katika utengenezaji wa silaha ni mfano wa kugeuzwa vikwazo kuwa fursa na kuongeza kuwa matukio hayo yamewashangaza maadui wote na yamekuwa kikwazo dhidi ya vitisho vya maadui.

Majibu ya kijeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Marekani kwa kulenga kituo chake cha kijeshi nchini Iraq baada ya Rais wa Marekani kuamrisha mauaji ya kiwoga dhidi ya Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iraq mwezi Januari 2020, na operesheni isiyo na kifani ya hivi karibui ya Iran ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya kambi za kijeshi za utawala haramu wa Israel zinatathminiwa katika muktadha huo.

Akichambua hali ya kiuchumi ya Iran licha ya vikwazo hivyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, pamoja na kwamba hatufichi taathira mbaya za vikwazo, lakini vikwazo hivyo vimepelekea kunawiri vipaji na kuibuka uwezo mkubwa katika sekta mbalimbali ambapo ustawi wa kiulinzi na uzalishaji ni mojawapo ya sekta hizi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akiashiria kushangazwa Wamagharibi kutokana na maendeleo ya silaha za Iran licha ya vikwazo vizito na vya kikatili, amesema kuwa, kwa uungaji mkono wa vikosi vya ndani vilivyojitolea na vilivyo na weledi, Mwenyezi Mungu akipenda, nchi itaendelea kustawi na kuendelea sio tu katika sekta ya ulinzi bali katika sekta nyingine zote.

Kwa mujibu wa Kiongozi Muadhamu, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sasa linajifaharisha kuwa linazalisha zana zote za ulinzi ndani ya nchi, na moja ya maeneo muhimu ya maendeleo ya kijeshi ya Iran ni kujitosheleza na kuboresha uwezo wa makombora, ndege zisizo na rubani na utengenezaji wa meli za kivita; zana ambazo sasa ni kizuizi dhidi ya vitisho vya maadui.

Kwa hakika licha ya kuwepo mashinikizo makubwa ya kisiasa na kiuchumi, Marekani na nchi za Magharibi hazijaweza kufikia malengo yao dhidi ya Iran, na chaguo la vikwazo vya silaha, kama vile vikwazo vya kiuchumi na kisiasa, halitafanikisha lolote kwa Marekani na Magharibi katika kukabiliana nayo.

Maendeleo katika sekta ya ulinzi kwa hakika yanachukuliwa kuwa kadhia ya kimkakati na katika sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hutegemea  wataalamu wa ndani ya nchi katika sekta za sayansi na teknolojia.

Wizara ya Ulinzi ya Iran imesisitiza mara kwa mara kwamba Jamhuri ya Kiislamu sio tu haina tatizo katika kuzalisha silaha za hali ya juu na za kistratijia, bali pia ustawi wa Iran katika sekta ya uzalishaji silaha ni mkubwa kiasi kwamba sasa Iran inauza bidhaa zake za ulinzi katika nchi mbali mbali duniani.

Tags