Mar 28, 2024 10:58 UTC
  • Marekani yaiwekea vikwazo GAZA NOW kwa tuhuma za kuchangisha fedha za kuisaidia HAMAS

Wizara ya Fedha ya Marekani imeiwekea vikwazo tovuti ya mtandao ya GAZA NOW kwa madai ya kuchangisha misaada ya kifedha kwan ajili ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS.

Kwa mujibu wa ABC News, wizara ya fedha ya Marekani imetangaza kwamba Ofisi ya Udhibiti wa Mali za Kigeni (OFAC) imewawekea vikwazo watu wawili na asasi tatu kwa hoja kwamba ndio warahisishaji wakuu wa njia za kuipatia fedha Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina, HAMAS.
 
Kwa mujibu wa tangazo la wizara ya fedha ya Marekani, GAZA NOW (Ghaza Sasa) na mwanzilishi wake Mustafa Ayash, pamoja na makampuni ya Al-Qureyshi Executive na Auzma Sultanah pamoja na mkurugenzi wa makampuni hayo mawili, wameshughulikia ukusanyaji wa misaada ya kifedha kwa ajili ya Hamas.
Wizara ya fedha ya Marekani

Tovuti ya Kiarabu ya Gaza NOW ina zaidi ya wafuasi 300,000 kwenye mtandao wa kijamii wa X na idadi kubwa ya wafuasi kwenye jukwaa la maongezi la Telegram.

 
Brian Nelson, naibu waziri wa fedha wa Marekani anayehusika na masuala ya kigaidi na taarifa za fedha amesema, wizara hiyo imedhamiria kuhakikisha inadhibiti uwezo wa Hamas wa kujidhaminia mahitaji ya fedha kwa ajili ya alichokiita 'shughuli zake za kigaidi', ikiwa ni pamoja na kupitia uendeshaji kampeni za kuchangisha misaada ya fedha.
 
Nelson ameongeza kuwa Marekani, ikishirikiana kwa karibu na mshirika wake Uingereza itaendelea kutumia nyenzo zote zinazohitajika ili kuvuruga uwezo wa Hamas kufanya mashambulizi zaidi.../

 

Tags