Apr 27, 2024 08:04 UTC
  • Kufuatia jinai za Israel, Gaza inahitaji miaka 14 kutegua mabomu na kuwa salama

Kwa muda wa karibu miezi saba sasa, utawala katili wa Israel umekuwa ukidondosha mabomu kila siku katika Ukanda wa Gaza na sasa Umoja wa Mataifa unasema zoezi la kutegua mabomu ambayo hayajalipuka eneo hilo linaweza kuchukua muda miaka 14.

Afisa Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma ya Uteguzi wa Mabomu UNMAS Pehr Lodhammar ameyabainisha hayo na kuongeza kuwa vita huko Gaza vimeacha ardhini takriban tani milioni 37 za mabomu. Amesema haiwezekani kubainisha kiasi halisi cha mabomu ambayo bado hayajalipuka katika eneo hilo ambalo hapo awali lilikuwa na idadi kubwa ya watu na wakazi zaidi ya milioni mbili lakini sasa limeharibiwa na kubakia vifusi baada ya takriban miezi saba ya mashambulizi makali kutoka Israel.

Mtaalamu huyo mkongwe wa Umoja wa Mataifa wa kutegua mabomu amesema kila mita ya mraba huko Gaza iliyoathiriwa na mashambulizi ya Israel ina takriban kilo 200 za vifusi. Akizungumza na waandishi habari mjini Geneva Uswisi jana Ijumaa amesema: "Ninachoweza kusema ni kwamba angalau asilimia 10 ya mabomu yanayodondoshwa hayalipuki ... tunazungumzia miaka 14 ya kutegeua mabomu."

Utawala dhalimu wa Israel ulianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza Oktoba 7, 2023.

Hali ya mtaa mmoja Gaza baada ya hujuma ya Israel

Hadi sasa zaidi ya Wapalestina 34,200 wameuawa shahidi na wengine 77,200 kujeruhiwa, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.

Kulingana na Umoja wa Mataifa zaidi ya miezi sita baada ya vita vya Israel, maeneo makubwa ya Gaza sasa ni magofu, huku asilimia 85 ya wakazi wa eneo hilo wakiwa wakimbizi wa ndani katika eneo hilo ambalo limezingirwa na kusababisha uhaba mkubwa wa  chakula, maji safi na dawa,

Afrika Kusini ilifungua kesi dhidi ya utawala wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ikiutuhumu utawala huo kuwa unatekeleza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Uamuzi wa muda wa mwezi Januari uliiamuru Israel kusitisha vitendo vya mauaji ya halaiki na kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba msaada wa kibinadamu unatolewa kwa raia huko Gaza. Israel ilipuuza uamuzi huo.