Apr 27, 2024 07:59 UTC
  • Mapigano yashadidi Sudan baina ya jeshi na RSF Sudan, watu 43 wauawa

Mapigano makali yameripotiwa Sudan jimboni Darfur Kaskazini, hususan mjini El-Fasher na viunga vyake, kati ya Jeshi la Kitaifa la Serikali SAF na wanamgambo wa RSF. 

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa Nairobi, Kenya, msemaji wa ofisi ya Kamishna wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Seif Magango amesema hali inazidi kuwa mbaya kwani katika kipindi cha wiki mbili zilizopita watu wapatao 43 wakiwemo wanawake na watoto wameuawa kutokana na mapigano kati ya pande mbili hizo hasimu.

Inaripotiwa kuwa pande zote zinarusha makombora kwenye maeneo ya raia, wengine wakitumia ndege za kivita kwenye makazi ya watu mjini El- Fasher na viunga vyake.

Hali hiyo imemtia hofu kubwa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk hasa kutokana na  kwamba wapiganaji wa RSF wanalenga vijiji vilivyoko magharibi mwa El-Fasher ambako wanaishi raia wa kabila la Zaghawa.

Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF)  linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.

Jenerali Abdel Fattah al Burhan (kulia) Hamdan Dagalo.

Hadi sasa juhudi za upatanishi wa kimataifa za kuhitimisha mapigano hayo na kuzishawishi pande hasimu kuketi kwenye meza ya mazungumzo zimegonga mwamba.

Hivi karibuni Justin Brady, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu (OCHA) nchini Sudan alisema, "leo, Sudan ni mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani. Nusu ya wakazi wa Sudan yaani watu milioni 25 wanahitaji msaada wa kibinadamu."

Aliongoza kuwa, "Mapigano ni makali sana kwa watoto, ambapo inakadiriwa watoto 730,000 wanaugua utapiamlo mkali," na kubaini kuwa, "Bila ya msaada wa haraka, zaidi ya watoto 200,000 wanaweza kufa kutokana na njaa inayotishia maisha katika wiki na miezi ijayo."