Apr 26, 2024 08:05 UTC
  • Mtaalamu wa UN ataka Israel iwekewe vikwazo vya silaha, mafuta

Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ardhi ya Palestina Inayokaliwa kwa Mabavu Francesca Albanese ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuweka vikwazo vya mafuta na silaha dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaoendeleza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Akizungumza siku ya Alhamisi Albanese ameikosoa Marekani na mataifa mengine ya Magharibi kwa kuhusika na uhalifu wa mauaji ya kimbari ya Israel kwa kuutumia utawala huo misaada ya kijeshi na silaha.

Aliongeza kuwa: "Ninachoweza kukuambia kwa uhakika ni kwamba msaada huu ni ukiukaji wa wazi, ni ukiukaji wa wazi wa amri ya muda ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) iliyoamuru kusitishwa vitendo ambavyo vinaweza kuwa sawa na mauaji ya kimbari na pia wito wa kufikishiwa Wapalestina misaada ya kibinadamu bila kizuizi chochote."

Mwezi Januari, kufuatia kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini, Mahakama Kuu ya Umoja wa Mataifa iliuamuru utawala wa Israel uchukue hatua zote kuzuia mauaji ya halaiki huko Gaza.

Albanese aidha amesema Umoja wa Ulaya unapaswa kuuwekea vikwazo utawala wa Israel na sio walowezi wenye itikadi kali pekee. Amesema walowezi wa Kizayuni wanatekeleza jinai zao kama sehemu ya sera za Israel za kupora ardhi za kihistoria za Palestina. Kwingineko katika maelezo yake, mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema  kwamba nchi za dunia lazima zifanye kila ziwezalo kuzuia mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.