Apr 28, 2024 12:03 UTC
  • Kan'ani: Sauti ya kuvurugika mifupa ya Uzayuni duniani inasikika zaidi hivi sasa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, sauti ya kuvurugika mifupa ya Uzayuni duniani inasikika zaidi sasa hivi kuliko wakati mwingine wowote.

Nasser Kanani Chafi, ameandika hayo kwenye mtandao wa kijamii wa X akizungumzia ukandamizaji mkali unaofanywa dhidi ya maandamano ya wanafunzi katika vyuo vikuu vya Marekani na Ulaya yanayofanywa kwa lengo la kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa wa Palestina na kusisitiza kuwa haiwezekani kuzuia kusambaratika nguzo zilizopasuka za ukaliaji ardhi ya Palestina kwa mabavu.
 
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa, 'hapana' kwa ukaliaji ardhi kwa mabavu wa Palestina, 'hapana' kwa mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza na kilio cha kukombolewa Palestina ndilo takwa linalopiganiwa duniani kote hii leo.

Maandamano ya wanachuo ya kuunga mkono Palestina na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni yaliyoanza katika Chuo Kikuu cha Columbia huko New York City, Marekani, licha ya kukabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa vyombo vya dola, yameenea kwanza katika vyuo vikuu vingine vya nchi hiyo, kikiwemo Yale, New York, Harvard, Texas, na Southern California na hivi sasa wimbi lake limesambaa hadi vyuo vikuu vya nchi nyingine za Magharibi, ikiwemo Ufaransa, Ujerumani na Uingereza pamoja na Canada na Australia.

Askari wa Marekani wakitumia mkono wa chuma kukandamiza mikusanyiko ya wanafunzo katika vyuo vikuu

Baada ya kupita zaidi ya miezi sita tangu utawala wa Kizayuni wa Israel uivamie Ghaza bila ya kupata matunda wala mafanikio yoyote, utawala huo unazidi kuzama kwenye kinamasi cha migogoro yake ya ndani na nje siku baada ya siku.

 
Katika muda wote huu, utawala katili wa Kizayuni haujapata mafanikio mengine isipokuwa ya kufanya jinai, mauaji, uharibifu, uhalifu wa kivita, kukiuka sheria za kimataifa, kushambulia mashirika ya utoaji misaada na kulinakamisha kwa njaa eneo la Ghaza.
 
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, tangu Oktoba 7, 2023 vilipoanza vita ya kinyama na mauaji ya kimbari ya utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Ghaza, hadi sasa watu elfu 34,388 wameuawa shahidi na wengine elfu 77,437 wamejeruhiwa.../

 

Tags