May 27, 2024 06:04 UTC
  • Iran yaanzisha mchakato rasmi wa uchaguzi wa rais

Iran imeanzisha mchakato wa uchaguzi wa mapema wa rais ambao umepengwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Juni wiki moja baada ya Rais Ebrahim Raisi kufa shahidi katika ajali mbaya ya helikopta kaskazini magharibi mwa nchi mnamo Mei 19.

Waziri wa Mambo ya Ndani Ahmad Vahidi alitoa amri siku ya Jumapili akiwaamuru magavana wa majimbo na miji kote Iran kuunda kamati kuu za uchaguzi ndani ya siku tatu zijazo.

Uchaguzi wa mapema wa urais unapaswa kufanyika kwa mujibu wa Kifungu cha 131 cha Katiba ya Iran ambacho kinasema kwamba rais mpya anafaa kuchaguliwa kwa kura za umma ndani ya siku zisizozidi 50 kuanzia siku ambayo rais anaaga dunia au kukosa uwezo wa kufanya kazi.

Baraza linalojumuisha wakuu wa mihimili mitatu ya serikali ya Iran lilifanya mkutano siku moja baada ya helikopta hiyo kuanguka na kukubaliana Juni 28 kuwa tarehe ya uchaguzi wa mapema wa rais nchini.

Makao Makuu ya Uchaguzi ya Iran yalitoa notisi ya kwanza Jumapili yakitangaza kwamba wagombea wanaweza kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi kati ya Mei 30 na Juni 3.

Baraza la Walinzi wa Katiba la Iran, chombo muhimu cha usimamizi wa kikatiba na kidini kinachohusika na usahihi wa uchaguzi, kitatangaza orodha ya wagombea walioidhinishwa wiki mbili kabla ya upigaji kura kuanza.

Ahmad Vahidi, Waziri wa Mambo ya Ndani

Kampeni zitaanza Juni 12 na kuendelea hadi Juni 27, kulingana na ratiba iliyotangazwa na serikali.

Helikopta iliyokuwa imembeba Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jumapili jioni Mei 19, 2024 ilipata ajali ilipokuwa ikirejea kutoka kwenye hafla ya ufunguzi wa bwawa la Qiz Qalasi kwenye mpaka wa pamoja wa Iran na Jamhuri ya Azerbaijan.

Wakati helikopta hiyo ilipokuwa inaelekea mji wa Tabriz, ilianguka katika eneo la Varzghan mkoani Azarbaijan Mashariki, kaskazini-magharibi mwa Iran. Ndani yake walikuwemo pia Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje, Imam wa Ijumaa wa Tabriz, Gavana wa Azarbaijan Mashariki na watu wengine; na wote pamoja wakapata hadhi tukufu ya kufa shahidi.