May 27, 2024 06:11 UTC
  • Kaimu Rais: Iran haitasitisha juhudi za kusaidia Sudan kustawi

Kaimu Rais wa Iran Mohammad Mokhber anasema Tehran haitasitisha juhudi za kusaidia Sudan kuweza kujitegemea, kupata maendeleo na amani.

Mokhber aliyasema hayo jana Jumapili alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Hussein Awad Ali, ambaye alifika Tehran kuwasilisha salamu zake za rambi rambi kufuatia kufa shahidi Rais Ebrahim Raeisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian na wenzao sita waliopoteza maisha katika ajali ya helikopta Mei 19.

Ameongeza kuwa, hayati rais na waziri wa mambo ya nje wa Iran walikuwa na nafasi nzuri katika kuhimiza uhusiano wa Iran na nchi za Kiislamu. Mokhber amesisitiza kuwa, hiyo ni sera ya kimsingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na itaendelea kutekelezwa.

Amebainisha kuwa sera za kistratijia za Iran zinatilia maanani matatizo yaliyopo katika mataifa na nchi za Kiislamu.

Mokhber ameishukuru serikali na taifa la Sudan kwa kuonyesha masikitiko yake na Iran kutokana na tukio  la kusikitisha la kufa shahidi Rais Raisi na wenzake.