Jul 15, 2016 04:12 UTC
  • Watalii wa kigeni waongezeka sana nchini Iran

Zaidi ya watalii 50 elfu wa kigeni wametembelea mkoa wa Isfahan wa katikati mwa Iran katika kipindi cha miezi minne iliyopita.

Shirika la habari la IRIB limeripoti habari hiyo na kumnukuu Bw. Fereydun Allahyari, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Mirathi ya Kiutamaduni, Sanaa za Mikono na Utalii ya mkoa wa Isfahan akusema kuwa, idadi ya watalii wa kigeni waliotembelea mkoa huo imeongezeka kwa asilimia 15 katika kipindi cha miezi minne iliyopita ikilinganishwa na muda kama huo mwaka jana.

Amesema, watalii hao waliotembelea mkoa wa Isfahan Iran kwenye kipindi hicho wametoka katika nchi 70 duniani kama vile Uhispania, Ufaransa na Ujerumani.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Mirathi ya Kiutamaduni, Sanaa za Mikono na Utalii ya mkoa wa Isfahan ameongeza kuwa, maeneo wanayopenda kuyatembelea sana watalii hao ni medani ya kihistoria ya Imam Khomeini (MA), bustani ya makumbusho ya Chehelsutun (nguzo arubaini) na Bagh-e Fin yaani Bustani ya Fin iliyoko Kashan, katikati mwa Iran.

Mkoa wa Isfahan wa Iran una vivutio 25 elfu vya kihistoria kwa ajili ya utalii na baadhi ya vivutio hivyo vimeorodheshwa kwenye Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO. Kwa mujibu wa UNESCO, Isfahan ndio mji mkuu wa kiutamaduni na kiustaarabu wa Iran ya Kiislamu.

Tags