Jun 21, 2024 02:16 UTC
  • Kani: Hatua ya Canada dhidi ya IRGC ni zawadi kwa Israel, magaidi

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hatua ya Canada ya kuliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC ) kwenye orodha ya kile inachokiita "makundi ya kigaidi" ni zawadi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, magaidi na maadui wengine wa amani na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi.

Sambamba na kulaani vikali hatua hiyo ya uadui ya serikali ya Canada dhidi ya Jeshi la IRGC, Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameeleza kwamba, kitendo hicho ni katika mfululizo wa hatua za Ottawa za kuuunga mkono utawala wa kigaidi wa Israel.

Katika ujumbe alioutuma jana Alkhamisi kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa X, Kani ameeleza bayana kuwa, jeshi la IRGC limekabiliana na magaidi na kuzima shari za magaidi katika eneo la Asia Magharibi.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ameeleza bayana kuwa, kwa hatua yake hiyo, Canada imeifuata kibubusa Marekani, ambayo mwaka 2019 ililiweka jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika orodha yake ya makundi ya kigaidi.

Mapema jana pia, Nasser Kanani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran alilaani vikali hatua hiyo ya kisiasa, isiyo ya kawaida na isiyo ya busara ya serikali ya Canada ya kulitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni la kigaidi.

Jeshi la SEPAH

Ikumbukwe kuwa, Januari mwaka huu, Bunge la Umoja wa Ulaya lilipitisha marekebisho ambayo yaliongezwa kwenye ripoti ya kila mwaka ya sera ya mambo ya nje, na kutaka nchi wanachama wake kuijumuisha IRGC katika orodha yao ya magaidi.

Hii ni katika hali ambayo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) ni taasisi ya kiutawala iliyotokana na muktadha wa taifa la Iran na ina utambulisho rasmi na wa kisheria unaotokana na Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu, ambayo, pamoja na vipengele vingine vya jeshi, ina jukumu la kulinda usalama wa taifa na mipaka ya Iran, pamoja na kuchangia kwa usalama imara na utulivu katika eneo ili kukabiliana na ugaidi.

Tags