Aug 04, 2024 02:23 UTC
  • Jumuiya ya Wayahudi wa Iran yataka kulipiza kisasi baada ya Israel kumuua Haniyeh

Jumuiya ya Wayahudi wa Iran imelaani vikali mauaji yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya kiongozi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) Ismail Haniyeh akiwa ugenini mjini Tehran, ikitoa wito wa kulipiza kisasi dhidi ya mauaji hayo.

Katika taarifa yake, jumuiya hiyo imelaani mauaji ya Haniyeh ikiyataja kuwa ni uhalifu wa kigaidi na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

"Kuuawa kwa Ismail Haniyeh, mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas akiwa Tehran, ni uhalifu wa kigaidi na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa," imesisitiza Jumuiya ya Mayahudi wa Iran.

Taarifa ya jumuiya hiyo imesema: “Shahidi Mujahid ambaye alikuwa mmoja wa wabeba bendera ya harakati ya ukombozi wa Quds Tukufu, alikaribia kuuawa shahidi mara nyingi, lakini hata baada ya kuwapoteza watu wa familia yake, hakuacha mapambano ya ukombozi na kuwatetea watu wanaodhulumiwa wa Gaza, na hatimaye ameuawa shahidi kwa shambulio la kihaini mjini Tehran."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Jumuiya ya Mayahudi wa Iran inatoa salamu za rambirambi kwa taifa shujaa la Palestina, wanamuqawa na Kiongozi Muadhamu [Ayatullah Sayyid Ali Khamenei] kutokana na mauaji ya Ismail Haniyeh, mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati ya Hamas, na inasubira kwa kiu kubwa jibu madhubuti na mwafaka kwa mauaji haya ya kihaini."  

Dk. Ismail Haniyeh

Dk. Ismail Haniyeh, ambaye alikuwa Tehran kuhudhuria hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian, aliuawa pamoja na mlinzi wake, katika shambulio la kigaidi lililotekelezwa na utawala katili wa Israel kwenye makazi yake kaskazini mwa Tehran mapema Jumatano iliyopita.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ameuambia utawala wa Israel ujitayarishe kwa "jibu kali" kwa mauaji ya Haniyeh na kueleza kuwa Jamhuri ya Kiislamu inapaswa kulipiza kisasi cha damu ya kiongozi huyo wa mapambano ya ukombozi wa Palestina.

Tags