Sep 09, 2024 14:47 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Mkono wa adui ni mtupu, tofauti na wanavyojigamba

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia vita vya kisaikolojia vinavyoendeshwa na maadui ili kuyaletea madhara mataifa huru na kusisitiza kuwa, tofauti na wanavyojigamba, mikono ya maadui ni mitupu na haina chochote cha maana.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumatatu hapa Tehran wakati alipoonana na maafisa wa Congress ya Taifa ya Mashahidi ya mkoa wa Kohgiluyeh na Boyer-Ahmad na kuongeza kuwa, moja ya misingi ya vita vya kisaikolojia vya maadui dhidi ya kila taifa na hasa hasa dhidi ya taifa letu la Iran ni kwamba maadui wanajigamba kupindukia na kujionesha wana nguvu kubwa katika kila kona; muda wote wanataka kuonesha kuwa, mataifa mengine hayana njia nyingine isipokuwa kuiogopa Marekani, kuwaogopa Wazayuni, kuiogopa Uingereza n.k, lakini uhalisia wa mambo ni kuwa, mikono ya madola hayo ya kibeberu ni mitupu na haina chochote.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, hivyo ni vita vya kisaikolojia vinavyoendeshwa na adui lakini wakati anapoingia kwenye mapambano fulani ya kijeshi, anakuwa mwepesi wa kukimbia.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesisitiza kuwa, katika uwanja wa kisiasa pia, adui anapenda sana kujionesha ana nguvu kubwa ili kuwafanya watu wengine wajihisi duni na wajione si lolote si chochote mbele ya madola hayo ya kibeberu. 

Ayatullah Khamenei amesema: Katika uga wa kiutumaduni pia, maadui wanajikuza kiasi kwamba wanawafanya watu wa mataifa mengine kuchukua maamuzi kwa pupa na kudharau mila na tamaduni zao na kuiga kibubusa tamaduni za watu baki na maajinabi.

Vilevile amesisitiza kuwa, moja ya mkakati mkuu wa Imam Khoimeini (MA) ulikuwa ni kufuta woga kwenye nyoyo za wananchi na kuyapa nguvu za kujiamini na kujithamini mataifa ya dunia.