Iran: Marekani na Uingereza ndio wachochezi wakuu wa vita duniani
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema Marekani na Uingereza ndio wachochezi wakuu wa moja kwa moja na wasio wa moja kwa moja wa kila vita vinavyotokea katika pembe yoyote duniani.
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imesema katika taarifa kwamba, kwa mujibu wa ahadi iliyotolewa na nchi hiyo mwezi Aprili uliopita kwa ajili ya kuongeza kasi ya kutumwa misaada ya kijeshi ya nchi za Magharibi kwa Ukraine, makombora ya ulinzi wa anga, vifaa vya ndege za kivita za F-16, silaha za AS90 na boti za kijeshi tayazi zimekabidhiwa kwa serikali ya nchi hiyo.
Taarifa hiyo imesema mamia ya makombora mapya ya ulinzi wa anga, makumi ya maelfu ya risasi za mizinga na magari ya kivita yatakuwa yametumwa Ukraine ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Kuhusiana na suala hilo, Nasser Kanani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa "X" akiashiria taarifa hiyo ya Wizara ya Ulinzi ya Uingereza kuhusiana na kuongezwa kasi ya kutuma silaha za nchi za Magharibi Ukraine kwamba popote palipo na vita duniani, nyayo za miguu ya Marekani na Uingereza huweza kuonekana kirahisi.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran aidha amekosoa hatua ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza ya kumuita naibu balozi wa Iran nchini humo kuhusiana na ripoti bandia ya kutumwa makombora ya Iran nchini Russia na kuongeza kuwa ripoti hiyo ilikuwa haijathibitishwa bado na kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tayari imeikanusha rasmi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilitangaza Jumatano katika taarifa yake ambayo nakala yake ilichapishwa kwenye tovuti ya serikali ya nchi hiyo, kwamba wizara hiyo kwa kuratibu mambo na washirika wake wa Ulaya na kwa amri ya moja kwa moja ya Waziri wa Mambo ya Nje, imemwita wizarani Ali Matinfar, naibu balozi wa Iran mjini London, ili kumlalamikia kuhusu suala hilo.
Viongozi wa Iran na Russia wamekanusha mara kwa mara madai ya kuwepo ushirikiano wa kijeshi kati yao kuhusiana na vita vya Ukraine na kuyachukulia madai hayo kuwa yasiyo na msingi wowote.